Habari za Punde

Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT) Watakiwa Kijiumarisha katika Kuwaunganisha na Kuwakwamua Wanawake

 

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi, wageni mbalimbali pamoja Wajumbe wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kabla ya kufungua Mkutano wa 10 wa Jumuiya hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 28 Novemba, 2022.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Samia Suluhu Hassan, ameutaka Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kujipanga upya kimkakati katika kujiimarisha kiuchumi, kijamii na kisiasa ili kutimiza malengo, dira na shabaha ya jumuiya hiyo, katika kutataua changamoto za wanawake nchini, sambamba na kuwafungamanisha katika kutumia fursa za kujikwamua na umasikini na kujiletea maendeleo endelevu.

 

Ndugu Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo (leo) Novemba 28, 2022 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa kumi (10) wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma ambao pamoja na mambo mengine utakuwa na ajenda ya uchaguzi wa viongozi wa jumuiya hiyo ngazi ya Taifa watakaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo (2022- 2027).

 

Amesema kumekuwa na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali za kuwaletea maendeleao wananchi katika nyanja za uimarishaji wa huduma mbali mbali za kijamii ikiwemo Maji safi na salama, Afya, Kilimo, ujenzi wa miundombinu ya kisasa pamoja na kuimarisha huduma za nishati ya umeme maeneo ambayo yanampa unafuu mkubwa mwanamke ili kuweza kufanya shughuli za maendeleo,

 

hivyo amewataka viongozi watakaochaguliwa kuwa kiungo kizuri baina yao na serikali hasa katika ufuatiliaji wa miradi hiyo ambayo inaligusa kundi kubwa la wanawake katika jamii.

 

“Wanawake katika historia ya Taifa letu waliunganisha watu wa rika zote na hadhi tofauti katika harakati za kudai uhuru, dhima hii ya kuwaunganisha watu ni yetu sisi wanawake, hatuwezi  kuikimbia kama vile ambavyo  hatuwezi kukimbia na kuziona familia zetu zikisambaratika. Mwanamke ni muhimili mkuu katika kuunganisha familia na jamii na vivyo hivyo ni lazima tubebe jukumu la kuunganisha, ili Chama chetu kiendelee kuwa madhubuti siku hadi siku” Alisema.

 

Kuhusu udhalilishaji wa kijinsia, Ndugu Samia Suluhu Hassan amewakumbusha UWT  kuendelea kupaza sauti zao  katika kupinga aina zote za udhalilishaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kutoa rai kwa ngazi zote kuanzia shina hadi Taifa ili kuondokana na vitendo hivyo ni vyema kushirikiana pamoja katika kupiga vita kwa  lengo la kupunguza maumivu na kuongeza furaha katika jamii.

 

Aidha, ameitaka UWT kuendelea kujipanga vyema katika kuimarisha jumuiya hiyo kiuchumi kwa kuwa na miradi ya uwekezaji yenye kwenda na wakati na kuisimamia vyema ili kuleta tija kwa taasisi hiyo ambayo ndio tegemeo kubwa katika ukombozi wa wanawake nchini kisiasa.

 

"Miradi tuliyonayo bado haijawa miradi mikubwa ya kutupa nguvu kubwa ya kiuchumi katika jumuiya. Kama mnavyojua uwezo wa kiuchumi hununua uwezo wa siasa, hivyo  tusiposimama vizuri na kwa sababu hatuna nguvu ya kiuchumi huenda tukanunuliwa kisiasa, twendeni kukajiimarishe na tukajipange vizuri ili kufikia lengo” Amesema.

 

Hata hivyo, Ndugu Samia Suluhu Hassan amezipongeza jumuiya za Chama Cha Mapinduzi (WAZAZI, UVCCM na UWT) kwa kukamilisha chaguzi katika ngazi zote ambapo amezikumbusha  kuwa jukumu kubwa liliko mbeleni ni kusimama na serikali katika kufanya shughuli za kujiletea maendeleo bila kujali itikadi za kisiasa na kwa kutanguliza Utanzania jambo ambalo litaendeleza ushirikiano, umoja na mshikamano wa Taifa.

  

      KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

 

                                  Shaka Hamdu Shaka

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM  Taifa

Itikadi na Uenezi.

28 Novemba, 2022

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.