Habari za Punde

Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar yashauriwa kutoa elimu ya sheria kwa jamii

 

Na Faki Mjaka-AGC,Zanzibar 07.01.2023

Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar imeshauriwa kuongeza juhudi ya utoaji wa elimu ya kisheria kwa jamii ili iweze kufahamu maswala mbalimbali ya kisheria.

Kwa kufanya hivyo Jamii ya wazanzibari itaweza kupata uelewa wa maswala ya kisheria na kuepuka kuingia katika hatia zisizo na ulazima.

Wito huo umetolewa na wananchi tofauti waliotembelea Banda la Maonesho la Afisi hiyo katika Tamasha la tisa la Biashara linaloendelea katika Viwanja vya Maisara mjini Unguja.

Mtumwa S. Kijiba kutoka Chukwani amesema muda umefika sasa kwa afisi hiyo kuvitumia vyombo vya habari kutoa elimu kupitia Wataalam wake waliobobea katika maswala ya kisheria.

“Hapa nimepata elimu iliyonifungua kichwa, natarajia kurudi tena kujifunza mambo mengi ila nivyema sasa mujipange kutufikishia taalumu hiyo kupitia vyombo vya habari ili watu wengi wanufaike” Alisema Kijiba

Kwa upande wake Abdallah S. Kinoo amesema elimu pia inahitajika hasa vijijini kulikosheheni migogoro ya ardhi hivyo ni vyema Afisi ya Mwanasheria Mkuu kuelekeza nguvu maeneo hayo.

Akijibu hoja na maswali kutoka kwa Wananchi hao Wakili wa Serikali kutoka Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar Salum Khamis Salum amesema Afisi hiyo imejiwekea utaratibu wa kutoa elimu ya sheria kwa wananchi (outreaches program) kila baada ya muda hasa katika maeneo ya vijijini ili kuongeza uelewa kwa wananchi.

Amefahamisha kuwa kila inapokaribia siku ya Sheria Afisi hiyo imejipangia utaratibu wa kufika maeneo tofauti ya Unguja na Pemba kutoa elimu kuhusu mambo mbali mbali ya kisheria.

“Pamoja na kuyachukua maoni yenu na kwenda kuyafanyia kazi ila ukweli utaratibu huo wa kutoa elimu upo hasa maeneo ya vijijini, tunafanya hivyo kipindi cha kuelekea maadhimisho ya siku ya sheria” Amesema Wakili Salum.

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya Tamasha hilo kwa ujumla wake Wakili Salum amesema watu wengi na rika tofauti huja katika Banda lao kuuliza maswali kuhusu kazi za taasisi na namna Afisi hiyo inavyotekeleza majukumu yake ya kila siku.

Hata hivyo amebainisha kuwa Idadi kubwa ya wananchi wamekuwa wakiulizia kuhusu kesi za migogoro ya ardhi na udhalilishaji jambo ambalo linaashiria kukithiri kwa mambo hayo katika jamii.

Hivyo amesema Afisi inapaswa kufikiria namna ya kutoa msaada na ushauri wa makusudi katika maeneo ya udhalilishaji na Ardhi ili kusaidia kupunguza matatizo hayo nchini.

Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar imeweka Banda lake katika Tamasha la tisa la Biashara linaloendea katika Viwanja vya Maisara mjini Unguja ili kuitumia fursa hiyo kutoa Elimu ya kisheria kwa wanachi wanaofika katika Banda hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.