RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema
amani, umoja na mshikamano ndio siri ya mafanikio yaliyopatikana ndani ya
kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya awamu ya nane.
Alieleza kufunguliwa kwa miradi ya
Maendeleo ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar kunatokana na kuwepo kwa mapenzi
makubwa ya wananchi kwa viongozi wao jambo alilolisisitiza kuendelezwa ili
Maendeleo zaidi yaongezeke kama ilivyo azma ya Serikali anayoiongoza.
Dk, Mwinyi alisema hayo kwenye ufunguzi
wa Hospital ya Wilaya, Micheweni kisiwani Pemba ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra
za miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alieleza
ufunguzi wa miradi kama hiyo ni kuyaenzi na kuyathamini Mapinduzi matukufu ya
Zanzibar ya mwaka 1964 na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kujenga Hospital katika
ngazi mbalimbali ikiwemo za Wilaya kama hiyo, Mikoa hadi Taifa.
Alisema ndani ya miaka mitano ya Uongozi
wake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kukamilisha haspitali zenye
ubora katika mikoa yote ambazo zitatoa huduma bora za Afya na hazitomfanya
mwananchi kusafiri nje ya nchi kufuata matibabu.
Dk, Mwinyi aliwataka watoa huduma za
Afya wakiwemo Madaktari, Wauguzi na wahudumu wa afya kuwa na lugha nzuri kwa
wagonjwa wanaowahudumia kwani lugha nzuri nazo ni tiba.
Naye Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui aliahidi kuwa Wizara hiyo itaendelea kusimamia na kutekeleza maagizo yote ya Rais kuhakikisha inakuwa na mageuzi kwenye utoaji wa huduma bora za matibabu ili wananchi wanapate huduma nzuri zaidi.
Hospital ya Wilaya ya Micheweni Pemba, ilikadiriwa kutumia zaidi ya shilingi billion 6 hadi kufunguliwa kwake na tayari imeshatumia zaidi ya shilingi Billion 5. Hospitali hiyo itatoa huduma mbalimbali muhimu za matibabu. zikiwemo chumba cha ICU, dharura, Vitanda vya kujifungulia na huduma za ICT.
No comments:
Post a Comment