Habari za Punde

Chuo cha Diplomasia chaaswa kutekeleza majukumu yake ya kimsingi

  

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akiongea na watumishi wa Chuo cha Diplomasia (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam  

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Diplomasia, Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi akizungumza  na watumishi wa Chuo cha Diplomasia (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam 

Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na watumishi wa Chuo cha Diplomasia kikiendelea Jijini Dar es Salaam 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akikabidhi vitabu kwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Diplomasia, Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi na Kaimu Mkuu wa CFR, Dkt. Felix Wandwe

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akikagua mradi wa ujezi wa madarasa ya kufundishia katika Chuo cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Chuo cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam

Chuo cha Diplomasia (CFR) kimeaswa kutekeleza majukumu yake ya msingi ili kukifanya chuo hicho kuwa kituo mahiri cha diplomasia.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) alipotembelea chuo hicho kilichopo Jijini Dar es Salaam na kuzungumza na watumishi wake.

Dkt. Tax amekitaka chuo hicho kifanye tafiti mahsusi za kusaidia utatuzi wa changamoto mbalimbali kwenye jamii hususani za kistratejia na kiintelijensia na kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa chuo hicho.

Amekitaka chuo kupanua wigo wa programu kutokana na ongezeko la wanafunzi ambao wanahitaji kujiunga na chuo hicho na kuandaa mpango wa kitaifa wa kutekeleza diplomasia ya uchumi. 

“Chuo kinapaswa kiongeze wigo wa mafunzo yake kama vile kutoa mafunzo ya strategia, kifanye tafiti mahsusi na kutoa ushauri kwa serikali na wadau wengine katika sehemu ya strategia na diplomasia,……….tafiti hizo zitachangia kuimarisha diplomasia na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabili changamoto zinazoikabili Serikali katika eneo hilo,” alisisitiza Dkt. Tax

Aidha, Dkt. Tax ameongeza kuwa, kila mhadhiri na mtumishi chuoni hapo anapaswa kuzingatia maadili na sheria kwani maadili ni sehemu muhimu katika eneo la kazi na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo wataweza kutoa wahitimu wenye maadili na tabia njema ambayo ni sifa kwa chuo.

Dkt. Tax pia amewahahakishia watumishi wa Chuo hicho kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na chuo hicho katika kuhakikisha kinaboresha mazingira yake ili kiendelee kuzalisha wanadiplomasia wabobezi watakao endeleza sifa nzuri ya chuo hicho nchini, kitaifa na kimataifa.

Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Diplomasia, Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi amesema chuo  hicho ni muhimu katika kutoa mafunzo ya uhusiano wa kidiplomasia na kuongeza kuwa kwa sasa chuo kinaendelea kuboresha muundo wake na mitaala ili kukifanya kuwa bora zaidi.

“Mhe. Waziri kwa sasa tuna jukumu la kukibadilisha chuo chetu kuwa taasisi ya kitaaluma na kimkakati, hii ni moja kati ya hatua za utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wakuu,” alisema Balozi Mwinyi.

Awali Kaimu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia, Dkt. Felix Wandwe alisema chuo kinaendelea kuandaa miundo mbalimbali ya kuboresha mazingira ya kufundishia na kuboresha mbinu za kuwanoa wanadiplomasia chuoni hapo.

Aidha, Dkt. Wandwe ameishukuru Serikali kwa kuendelea kukilea chuo hicho na kukiwezesha kuzalisha wanadiplomasia wazalendo wanaopeperusha vyema bendera ya Tanzania kitaifa na kimataifa. 

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Wangwe aiomba Serikali kukiwezesha chuo hicho kutatua changamoto ya wakufunzi wa masomo ya lugha za kigeni hususan Kireno na Kifaransa. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.