Habari za Punde

Wanawake Zanzibar Watakiwa Kujifunza Utengenezaji wa Batiki

Na Maulid Yussuf WMJJWW Zanzibar 

Waziri wa  Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma  amewataka wanawake wa Zanzibar kujifunza juu ya utengenezaji wa mabatiki ili kuweza kujiinua kiuchumi.

Amesema hayo katika maadhimisho ya siku ya batiki Zanzibar  iliyofanyika katika viwanja vya maonesho Maisara Mjini Unguja.

Amesema wanawake wanapaswa kupewa mafunzo juu ya utengenezaji wa batiki ili kuwawezesha kujikwamua  na kuisaidia Serikali katika kuongeza mapato.

Waziri Pembe amesema ni vyema kupewa ujuzi kwa wwnawake hao ili kuweza kuwaunganisha  na kuwa wamoja kati ya Moro batiki na Zanzibar batiki ili kutengeneze batiki za  kiwango cha hali ya juu na zilizokuwa na ubora sawa.

Aidha Mhe.Riziki ameziomba  Tasisi za Serikali na binafsi  kuweka oda za Batiki wanapokuwa na shughuli zao mbalimbali kwa lengo la kuwaunga mkono wafanya biashara hawo wadogo wadogo na  kuweza kuletea maendeleo.

Nae Katibu  Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya viwanda bwana Ali Khamis Juma amesema, soko la batiki kwa Zanzibar ni kubwa kwa wafanya biashara watakao weza kutengeneza batiki.

Amesema wapo wafanya biashara wengi wadogo wadogo wanajiunga na ujasiriamali lakini wengi wao  si wajasiriamali kwani wanakuwa wanafuata mkumbo tu.

Hivyo amewataka wajasiriamali wadogo kujitahidi  kutengeneza mabatiki hayo na kuweza kuuza kwa watalii ili kujiingizia kipato wao wenyewe pamoja  na kuongeza pato kwa Serikali.

Hata hivyo amesema maazimio yaliyofikiwa katika maadhimisho hayo yatasaidia kufikia katika malengo yao waliyojiwekea katika kujikwamua na umasikini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa  Moro batiki Group Dr Herriet James Mkanga, amewataka wanawake kujishughulisha na ujasiriamali kwa kujiunga na vikundi ili kujikomboa na umasikini.

Amesema lengo lao ni kutoa ajira kwa wanawake na vijana ili kuweza kujikimu mahitaji yao ya kila siku.

Amesema wapo katika kutengeneza bidhaa zenye ubora ili kuitangaza Tanzania katika nchi za Kimataifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.