Habari za Punde

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto akutana na kufanya kikao maaluim na Shirika la Kimataifa la Wazee Duniani HELPAGE

 Na Maulid Yussuf WMJJWW 


Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe Riziki Pembe Juma amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inashukuru kwa mashirikiano mazuri ya shirika la Wazee Duniani Helpage katika kuwapatia maendeleo wazee wa Zanzibar. 

Mhe Riziki amesema tokea Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar,  Serikali inaendelea kuwatunza Wazee waliopo kwenye makaazi ya Wazee Sebleni, Welezo na Limbani Pemba.

Mhe Riziki amesema hayo wakati wa kikao maalumu cha Majadiliano kati ya Wizara yake na Shirika la Kimataifa la Wazee Duniani HELPAGE kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Nchi, Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mwanakwerekwe Mjini Unguja.

Amesema hivi karibuni kuna Makubaliano yamefanyika na Umoja wa Falme za Kiarabu U.A.E, ili kufanya ukarabati majengo ya makaazi ya wazee Welezo kwani yapo katika hali ya uchakavu na kutumia fursa hiyo kuwakaribisha Shirika hilo ili kama litaweza kufanya ukarabati majengo ya Sebleni na Limbani.

Hata hivyo amesema Serikali itaangalia uwezekano wa kuongeza kiwango cha fedha inayotolewa kwa wazee endapo uchumi utaruhusu kwani mripuko wa maradhi ya UVIKO 19 yalioitikisa dunia nao umepelekea kushuka kwa kipato ndani ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Hata hivyo amesema, Wizara inafanya kazi kwa karibu sana na Wizara ya Afya katika kuwashughulikia wazee waliopo katika makaazi wakati wanapohitaji huduma hizo za matibabu.

Nae Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Kimataifa la Wazee Duniani kanda ya Tanzania bwana Smart Daniel amesema Helpage ipo tayari kutoa mashirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakati wowote watakapohitajika. 

Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni Maendeleo ya Sera Bi Shekha Mohammed Ramia amesema, Shirika la Helpage linaendelea kuiwezesha Zanzibar kwa miaka mingi kwa kutekeleza miradi ya kuwasaidia wazee.

Amesema Helpage kwa kushirikiana na UNICEF imeandaa mfumo wa Kumbukumbu ya Pencheni Jamii pamoja na kuwezesha kuandaliwa kwa sheria namba mbili ya wazee ya mwaka 2020 pamoja na kanuni mbili ya makaazi na Pencheni jamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.