RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameihakikishia dunia kwamba Zanzibar ipo
salama haina viashiria vyovyote vya kutishia amani kwa wenyeji na wageni
wakakaoitembela.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo alipofungua maonesho ya Utalii na Uwekezaji kwenye ukumbi wa Makumbusho ya Beit
el Aman, Mnazi Mmoja - Zanzibar.
Alisema maonesho
hayo yatatoa mchango mkubwa wa kukuza sekta ya utalii Zanzibar na kuwaomba
wageni na watalii kutoa shaka kwa kutembelea visiwa vya Unguja na Pemba
kuangalia mandhari nzuri na vivutio vya utalii vilivyomo.
“Nachukua
nafasi hii kuihakikishia dunia kwamba Zanzibar ni salama hakuna tukio au
viashiria vyovyote vya kutishia usalama wa wageni na wenyeji, kwa wale wote waliopanga kuitembelea nchi
yetu tunawakaribisha na wale ambao bado hawajafanya maamuzi ya wapi watembelee,
basi nawashauri waichague Zanzibar iwe ni sehemu yao ya mapumziko kwa msimu
huu” Alieleza Dk. Mwinyi.
Alisema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ziko
imara kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama na yenye amani kwa wenyeji na
wageni wanaoitembelea.
Rais
Dk. Mwinyi alieleza, mwishoni mwaka jana jumla ya watalii 548,503
waliingia Zanzibar ikilinganishwa na wageni 260,644 waliongia mwaka 2020
kufuatia athari za janga la UVIKO-19 lililoathiri sekta ya utalii nchini na
dunia kwa ujumla na kuongeza Zanzibar kama sehemu ya dunia iliathirika kwa shughuli
zote za utalii zilisimama kwa takriban miezi saba kuanzia mwezi Machi mwaka 2019. Alielza hali sasa inaendelea
kuimarika kwa watalii wengi kuingia nchini.
Dk. Mwinyi aliitaka
Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kupitia Kamisheni ya Utalii kushirikiana na
Jumuiya za wafanyabiashara za utalii kujipanga upya na hatimae kuja na mpango
madhubuti wa kuzitumia fursa za biashara ya utalii zilizopo Zanzibar. Aidha,
aliipongeza Wizara hiyo kwa kazi nzuri ya kuimarisha Utalii nchini. Sambamba na
kuwahimiza kuongeza ubunifu wa kuibua vivutio vipya ikiwemo utalii wa matamasha,
mikutano ya kimataifa, makongamano na utalii wa michezo ya baharini.
Pia aliishukuru
sekta binafsi kwa kuendelea kutangaza utalii wa Zanzibar pamoja na kutoa huduma
nzuri zinazosaidia kuitangaza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Alisema
ushirikiano wa pamoja unahitajika baina ya Serikali na sekta binafsi kwa
kufanyakazi pamoja katika kuzitumia vyema fursa za biashara ya utalii
zilizopo nchini.
“Natoa
pongezi na shukrani kwa Balozi zetu zote zilizo nje ya nchi kwa kufanya juhudi
kubwa za kuvutia watalii kuja nchini” Alipongeza Rais Mwinyi.
Akizungumzia
utalii endelevu na umuhimu wa kutunza mazingira, Rais Dk. Mwinyi alieleza
maonesho hayo pia yanalenga maudhui ya Zanzibar ya kijani yenye
kusadifu utalii endelevu wenye urithi tofauti wa kimaumbile, utamaduni na
historia hai pamoja na kuonesha uwiano uliopo baina kutunza mazingira hai,
uchumi, jamii na utamaduni ambao ni
muhimu kwa maendeleo ya sekta ya utalii na uhifadhi wa mfumo wa ikolojia.
Alisema, dhamira ya Serikali ni kutunza mazingira na kuhakikisha shughuli
za utalii na uwekezaji zinaekewa
mikakati mizuri ili kulinda mazingira na utamaduni za wazawa kwa kuongeza
mapato yatokanayo na sekta ya utalii na uwekezaji nchini.
Hata hivyo, Dk.
Mwinyi aliwataka wageni waliopo nchini kufurahia ukarimu wa watu wa Zanzibar
pamoja na kuwataka kuwa mabalozi wazuri watakaporejea kwenye mataifa yao kwa
kueleza mambo mazuri waliyoyashuhudia Zanzibar.
Naye, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale.Mhe. Simai Mohammed Said aliwataka
wananchi wa Zanzibar kupenda kununua na kutumia bidhaa zinazozalishwa na
kutengenezwa nchini ili kuzifanya pesa kuendelee
kuzunguruka na kuongeza uzalishaji.
“Tukifanya hivyo thamani ya pesa itaendelea kubakia ndani itazunguruka kwa
watu wetu, tuekeze sana na kutengeneza fedha nyingi ili kuboresha maisha ya
watu kwaalili ya maisha mazuri kwao yatokanayo na faida ya utalii, Zanzibar”
Akizungumzia miundombinu ya mawasiliano na barabara, Waziri Simai alieleza barabara
nyingi za mji wa Zanzibar hazivutii kwa utalii, hivyo alizishauri mamkala
husika kwa sasa waziboreshe na kupanda miti, bustani na maua mengi kwaajili ya
kuwavutia wageni wanaofika nchini kwa uzuri na mvuto wa mwonekano wa kijani na
maua hivyo aliwashauri Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja nawadau wa Utalii
kuishawishi jamii juu umuhimu wa kuzitunza na kuzienzi barabara na maeneo yote
ili Zanzibar iboreke na kuwa na mvuto wa kipekee kwa watalii.
Waziri Simai alielekeza miti mingi ipandwe kwenye barabara kuu za miji,
ambako watalii wengi hupita na kuona mandhari halisi ya mji wa Zanzibar.
Alimuahidi Rais Dk. Mwinyi kwamba watashirikiana na taasisi nyengine za
serikali zikiwemo Wizara ya utalii,
usafirishaji na mawasiliano, Ardhi, Afya na wadau wengine wa utalii kufanya
kazi kama timu moja ili kuungamkono jukudi za serikali kwenye kufikia lengo la
utalii endelevu nchini na kufanikisha malengo ya utalii kwa ajili ya kizazi
kijacho
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Rahim Baloo
aliyataka mashirika ya ndege ya kimataifa kuungamkono juhudi za Serikali kwa
kuongeza safari za moja kwa moja kutoka mataifa makubwa kutua Zanzibar hali aliyoieleza
itaifungua Zanzibar kwenye soko la kimataifa la utalii.
Alisema maonesho hayo yataifungulia milango Zanzibar kwenye soko la
kimataifa hadi kwa mataifa ya kusini na kaskazini mwa bara la Amerika.
Maonesho hayo ya siku tatu yanatarajiwa kuhudhuriwa na
zaidi ya washiriki 200 kutoka mataifa mbalimbali zikiwemo nchi za Algeria,
Argentina, Brazil, Marekani na kwengineko.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment