Habari za Punde

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Dimwa Ziarani Pemba na Maelfu Wajitokeza Kumpokea

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohammed Said Mohamed (Dimwa),akiongoza matembezi ya msafara wa Sekretarieti ya NEC Taifa Zanzibar  kuelekea katika Afisi ya CCM kitengo cha uratibu Chachani Chake Chake Pemba.
 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohammed Said Mohamed (Dimwa),akivishwa skafu mara baada ya kuwasili katika Afisi ya uratibu wya Chama Cha Mapinduzi Pemba.
 NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM) Zanzibar Dkt.Mohammed Said Mohamed (Dimwa) akimsalimia mmoja wa Wazee wa CCM Kisiwani Pemba alipofika kumtembelea na kumjulia hali yake, wakati wa ziara yake ya Kikazi iliyoaza leo.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohammed Said Mohamed (Dimwa), akizungumza na Wananchi wa kisiwa cha Pemba mara baada ya kuwasili katika Afisi ya uratibu Pemba.

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk. Mohammed Said Mohammed 'Dimwa',amesema hakuna mtu yeyote mwenye hati miliki ya Chama hicho bali ni Chama cha watu wote.

Alisema wakati umefika wa Chama hicho kurudi kwa wanachama wenyewe ili waamue masuala mbalimbali yenye tija ya kisiasa na kiuchumi.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na maelfu ya Wanachama wa Chama hicho huko katika Afisi ya CCM ya Kitengo cha uratibu Chachani Chake Chake kisiwani Pemba.

Alisema CCM itashuka kwa wananchi kuhakikisha wanajengewa uwezo kupitia madarasa ya itikadi kwa lengo la kujiimarisha kisiasa kuanzia ngazi hizo zenye wanachama wengi.

Dkt. Dimwa, alitumia nafasi hiyo kuwaonya baadhi ya wanasiasa na wanachama wa vyama vya upinzania nchini kuacha kauli za uchochezi wa vurugu na badala yake wajielekeze katika kudumisha amani na mshikamano.

 Alisema, kumeanza kujitokeza maneno ya choko choko na kwamba CCM msimamo wake ni kujibu maneno hayo kupitia usimamizi wa utekelezaji wa Ilani yake ya mwaka 2020/2025 inayotekelezwa kwa kasi kubwa na Serikali zote mbili ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kazi yetu kubwa ni kuwahudumia wananchi waliotupa kura za kuongoza dola, hatuwezi kukatishwa tamaa na kauli za baadhi ya wasioitakia mema CCM.

Alisema, serikali ya Umoja wa Kitaifa SUK inatambuliwa ndani ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984,hivyo wasioridhika wana nafasi ya kufuata taratibu ili kama kuna changamoto zitatuliwe.”,alisema Dimwa.

Aidha aliwatataka viongozi na wanachama wa CCM kuwa na mipango kazi inayoendana na mikakati ya kuimarisha Chama hicho.

"Naamini kuwa Chama cha Mapinduzi 2025 kitashinda kwa kishindo tena saa nne asubuhi kwani tuliyoahidi tunaendelea kuyatekeleza kwa vitendo”.alifafanua Dkt.Dimwa.

Katika maelezo yake Dkt.Dimwa, alisema CCM itafanya siasa za kisayansi kwa kuhakikisha kila mwanachama ananufaika na fursa zinakazopatikana kupitia taasisi hiyo kubwa ya kisiasa.

Aliwatoa hofu baadhi ya wananchi wanaokosoa maamuzi ya Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuruhusu mikutano ya hadhara kwani Viongozi wa Chama na Jumuiya zake wana uwezo wa kujibu hoja hizo kwa ufasaha.

"Sisi hatuwezi kujibu maneno ya khanga bali tutawajibu kwa hoja, ndani ya miaka miwili CCM imefanya mambo makubwa sana haija wahi kutokea hivyo tuna mengi ya kuwajibu wapinzani kwa maendeleo yaliyofanyika kwa kipindi kifupi," alisema.

Alisema, Dkt.Dimwa kuwa ana kazi mbili kubwa kwanza ni kumtetea Mwenyeti wa CCM, kumsemea lakini na kumlinda, na kazi yake ya pili ni kumlinda na kumsemea  Makamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Mwinyi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba, Yussuf Ali Juma aliahidi kutoa ushirikiano na kutekeleza maelezo yote yaliyotolewa.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba Inocent Nyanzaba, alisema hali ya kisiasa ndani ya Mkoa huo ipo vizuri.

Aidha alisema, kuna mahusiano mazuri ya Chama cha Mapinduzi na Jumuiya zake na kwamba pale panapotokea changamoto basi mamlaka husika kwenye ngazi hizo huzitatua.

Mapema Mkuu wa Mkoa huo Mantar Zahor Masoud, alisema kwamba ndani ya Mkoa huo wametekeleza kwa ufanisi Ilani ya CCM kwa kuimarisha huduma za afya,maji,elimu,uvuvi,kilimo,biashara na mindombinu ya usarifi wa anga nan chi kavu.

Alieleza kwamba katika juhudi za kuwawezesha wananchi kiuchumi serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni nne kwa ajili ya mikopo ya kuviwezesha vikundi 45.

Zahor, alisema pamoja na mafanikio hayo wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa huduma za maji safi na salama kwa baadhi ya maeneo, changamoto hiyo ina sababishwa na umeme kuwa na nguvu ndogo za kuendesha mitambo ya maji.

Akijibu hoja hiyo, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Khamis Mbeto Khamis, alisema CCM tayari imeanza kuchukua juhuzi za kuzungumza na viongozi wa TANESCO ili wakutane na viongozi wa ZECO kwa ajili ya kumaliza changamoto hiyo kisiwani Pemba.

Viongozi wanaounda Sekretarieti hiyo ya NEC Taifa Zanzibar waliofanya ziara hiyo ya kujitambulisha Pemba ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohammed Said Mohammed,Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Organazesheni Omar Ibrahim Kilupi na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis.

Wengine ni Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Khadija Salum Ali na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya uchumi na fedha CCM Zanzibar Afadhali Taibu Afadhali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.