Habari za Punde

RAIS SAMIA ATOA SULUHU MGOGORO WA ARDHI KINGALE - KONDOA

 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza na wananchi wa Vijiji vya Kingale katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa na Gereza la King'ang'a ambao wamekuwa kwenye mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miongo mitatu dhidi ya eneo lenye ukubwa wa ekari 7,495.74. Mwishoni mwa wiki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa Suluhu ya mgogoro huo kwa kuzingatia mahitaji ya Wananchi.


Wananchi wa Vijiji vya Kingale katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa na Gereza la King'ang'a wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule mara baada ya kuwasilisha suluhu ya mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miongo mitatu katika eneo lao. Mwishoni mwa wiki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa Suluhu ya mgogoro huo kwa kuzingatia mahitaji ya Wananchi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa Suluhu kwenye mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miongo mitatu dhidi ya eneo lenye ukubwa wa ekari 7,495.74 lililopo katika Vijiji vya Kata ya Kingale katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa na Gereza la King'ang'a ambalo ni eneo lenye rutuba kwa shughuli za kijamii za uzalishaji.

Suluhu hiyo imewasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule kwa niaba ya Mhe. Rais na ameitoa mbele ya wananchi wa Kata hiyo wakiwa na viongozi wao.

"Ardhi yote ni mali ya Serikali, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alipofika hapa alifikisha hili jambo kwa Mhe Rais aamue na Rais ametoa suluhu kwa Wanakingale. Amesema eneo lenye mgogoro la ukubwa wa ekari 7,495.74, ekari 3,272.4 zibaki kwa wananchi watumie kwa shughuli za kilimo, mifugo na za kiuchumi na Magereza watachukua ekari zilizobaki" amesema Mhe. Senyamule

Mbali na kuwasilisha utatuzi pia Mhe  Rais ameagiza mambo kadhaa yafanyike katika eneo hilo; "Mhe. Rais ameagiza kuwa ndani ya mwezi mmoja, watu wa ardhi waje kuonyesha utaratibu wa maeneo yaliyogawanywa, yapimwe na alama ziwekwe zinazoonekana kwa kila mmoja. Vijiji tuendelee kutunza mipaka kuzuia mwingiliano wa matumizi, Magereza pia mtunze mipaka, wananchi wapo upande wa Bonde linalofaa kwa umwagiliaji. Wizara ya Kilimo mfanye utaratibu wa kujenda mabwawa kwa ajili ya umwagiliaji, mifungo pia mjenge majosho kwa ajili ya kuosha mifungo ya wananchi" Ameongeza Mhe. Senyamule

Kadhalika, Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi hao kufanya maendeleo kwa kushirikiana na Magereza kwani mgogoro umekwisha hivyo kutokana na miundombinu itakayojengwa kwenye eneo hilo, itawawezesha kupiga hatua kubwa kwa haraka na kumfanya Mhe. Rais kujivunia kuwapatia eneo hilo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mji Mhe. Ally Makoa amesema mapendekezo ya ya kupatiwa eneo waliloomba kutoka kwenye mpaka wa Magereza waliyowasilisha kwa Rais, ndicho kilichoamuliwa hivyo wananchi hao wataendelea kutumia eneo lao la mashamba huku Magereza nao wakibaki na eneo lao. Hakusita kutoa pongezi zake kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta wataalamu kutoka Wizarani kwa ajili ya kujenga miundombinu kwenye eneo hilo pamoja na kuridhia mapendekezo ya wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.