Dodoma, 15 Februari 2023
Tanzania imekabidhiwa rasmi uenyekiti wa Sekta ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu
katika Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) kwenye hafla
fupi iliyofanyika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo yaliyopo jijini Brussels,
Ubelgiji tarehe 13 Februari 2023.
Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, kwenye Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya OACPS, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga alikabidhiwa rasmi Uenyekiti wa Sekta hiyo kwa ngazi ya mabalozi na Balozi wa Ghana nchini Ubelgiji, Mhe. Harriet Sena Siaw-Boateng ambaye nchi yake imemaliza muda wa uenyekiti.
Uamuzi wa Tanzania
kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa sekta hiyo ulifikiwa katika Mkutano wa Baraza la
Mawaziri wa Nchi Wanachama wa OACPS uliofanyika Brussels, Ubelgiji, Mwezi Juni
2022. Uenyekiti
wa Tanzania utakuwa kwa ngazi mbili ambazo ni za Mabalozi wa Jumuiya waliopo
Brussels na Mawaziri wenye dhamana ya sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu ndani
ya Jumuiya na utadumu kwa miaka miwili hadi Februari 2025.
Tanzania katika kipindi cha uongozi wake imejipanga
kikamilifu kusimamia utekelezaji wa masuala mbalimbali katika Jumuiya ikiwa ni
pamoja na kuweka mikakati madhubuti na mazingira ya kuwezesha wananchi kupitia
nchi zao kunufaika ipasavyo na uchumi wa buluu ikiwemo uvuvi na rasilimali
zingine za majini; kuchochea uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu; kujenga
uwezo na matumizi bora ya sayansi na teknolojia; kuongeza wigo wa masoko kwa
bidhaa zitokanazo na uvuvi na uchumi wa buluu; kupambana na uvuvi haramu; na
kuendeleza juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, katika kipindi husika, Tanzania itakuwa na
jukumu la kuandaa Mkutano wa Mawaziri wa
OACPS wenye dhamana ya masuala ya Uvuvi ambao unatarajiwa kufanyika nchini
Tanzania mwaka 2024.
Miongoni mwa sababu zilizopelekea Tanzania
kuchaguliwa katika nafasi hiyo ni kutokana na kuongozeka kwa ushawishi wake
ndani ya Jumuiya ya OACPS na kuthamini utayari, dhamira na hatua thabiti
zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuchochea
na kusimamia masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ikiwemo yale yanayohusu
sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu kwa ujumla.
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali.
No comments:
Post a Comment