Habari za Punde

Zoezi la kuwahamasisha wanawake kujitambua na kujiinua kiuchumi nchini laendelea

 Na Maulid Yussuf WMJJWW 

 

Katika shamra shamra za kuadhimisha siku ya wanawake Duniani, Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto inaendelea na zoezi la kuwahamasisha wanawake kujitambua na kujiinua kiuchumi nchini.

Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto bi Siti Abbas Ali amefika katika kambi ya Jeshi la Kujenga Uchumi JKU Mtoni na kuwapa elimu juu ya masuala ya udhalilishaji pamoja na kujitambua kwa Wanafunzi wanaojifunza uzalendo na ukakamavu katika jeshi hilo.

Bi Siti amewataka wanawake kushirikiana na kusimama imara katika kuhakikisha wanafanya kazi zote bila ya kujali jinsia zao ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Amesema hakuna kazi maalumu za wanaume wala kazi maalumu za wanawake, ni lazima kuwa imara na kukubali kuwa kazi zote wanawake wanaweza.

Amesema Serikali ilipoamua kumuinua mwanamke katika ngazi mbalimbali sio kama imekosea,  bali inataka wanawake waweze kujitegemea kwa kujiajiri wao wenyewe bila ya kusubiri ajira kutoka Serikalini. 

"Wanawake shikamaneni, uganeni na shirikianeni kuona kila penye mwanamke kuhakikisha anafanikiwa, na msiwekeane choyo wala roho mbaya, kwani hamtafanikiwa" amesisitiza Mkurugenzi Siti.

Aidha amewataka wanaume kuwasaidia wanawake kuhakikisha wanafanikiwa kwani watu wote ni sawa kama katiba ya Zanzibar inavyoeleza.

Naye Mwalimu katika Skuli ya Ufundi JKU na  Sekondari , Meja Halima Khamis Khatib ameiomba Idara kuwa na muendelezo wa kufika katika Jeshi hilo kuwapa elimu vijana kwani kila mwaka wamekuwa wakipokea  wanafunzi wapya na wa rika na tabia tofauti, hivyo imani yao elimu hiyo itaweza kuwasiadia vijana hao kwa kuondokana na ushawishi wa matendo ya udhalilishaji. 

Kwa upande wao Wanafunzi wa Jeshi la kujenga uchumi Zanzibar JKU wameishukuru Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto kwa uamuzi waliouchukua wa kuwapatia elimu ya kujitambua pamoja  na masuala ya udhalilishaji na kuwaomba waendelee ili kuwasaidia kujua mbinu za kukabiliana na matatizo mbalimbi katika maeneo yao.

Wamesema katika jamii wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali juu ya masuala ya udhalilishaji lakini elimu hiyo imewapa mwamko wa kujitambua pamoja na kujua namna gani watajikwamua na changamoto hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.