RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesifu maendeleo makubwa ya
kiuchumi yaliyofikiwa na Ufilipino kupitia sekta mbalimbali.
Alisema Zanzibar ina mengi ya
kujifunza kwa Ufilipino kutokana na uzoefu na weledi wa kuyafikia maendeleo
hayo hasa kwenye sekta za mafuta na gasi, utalii, uvuvi na afya.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu,
Zanzibar alipozungumza na balozi wa Ufilipino nchini Tanzania, Marie Charlotte
aliyefika kujitambulisha.
Rais Dk. Mwinyi alisema Utalii ni
sekta mama kwa uchumi wa Zanzibar na kumshauri Balozi Charlotte kuangalia fursa
za uwekezaji kwenye sekta hiyo kwa kuitangaza zaidi Zanzibar huko kwao.
Alisema, Zanzibar ina idadi ndogo
ya raia wa Ufilipino, hivyo alimueleza balozi huyo matarajio yake kuona
ushirikiano uliopo unaimarika zaidi kwa kuongezeka raia wengi wa Ufilipino,
Zanzibar.
Vile vile, Rais Dk. Mwinyi
alimueleza Balozi huyo kwamba Zanzibar inawakaribisha raia wa Ufilipino kuja
kuwekeza kwenye sekta ya Uchumi wa Buluu kwani ina mawanda mapana ya uwekezaji
na faida kubwa kwa pande zote mbili za ushirikiano.
Naye, Balozi Charlotte alimueleza
Rais Dk. Mwinyi wataongeza uhusiano wa kidiplomasia ulipo baina ya Tanzania na
Ufilipino, nakusema kwamba ataitangaza Zanzibar kwa kusawishi wawekezaji kutoka
nchini kwake kuwekeza Zanzibar kutokana na fursa zinazopatikana kwenye visiwa
vyake.
Pia balozi huyo, aliisifu Zanzibar
na kusema mazingira yake yanafanana sana na Ufilipino na alishangazwa na
utamaduni wa watu wa Zanzibar kwa ukarimu wao kwa wageni, unatofautiana kidogo
na ule wa Wafilipino.
Uhusiano wa Diplomasia baina ya Tanzania na
Ufilipino ulianza tangu Disemba 15 mwaka 1961 kwa pande mbili hizo kufungua
ofisi za kidiplomasia na kushirikina kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo,
jamii na uchumi.
Ufilipino mji mkuu wake Manila, iko Kusini
Mashariki mwa bara la Asia, ni nchi ya visiwa Magharibi mwa bahari ya Pasifiki,
ina visiwa vidogo 7,641, inachangia mipaka na bahari ya China.
IDARA YA MAWASILIANO
IKULU, ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment