NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohammed Said Mohammed ‘Dimwa’,amesema Chama Cha Mapinduzi haitowavumilia baadhi ya wanachama,makada na watu wanaokwamisha juhudi za Wabunge,Wawakilishi na Madiwani kwa kubeza na kukejeli miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa majimboni.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa uzinduzi wa kisima cha maji safi na salama kilichopo shehia ya Karakana Jimbo la Chumbuni,Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alisema kuna baadhi ya wanachama wanaonyemelea nafasi za uongozi katika majimbo wameanza kujipitisha kwa wananchi wakitoa kauli zisizofaa za kubeza miradi ya maendeleo inayotekelezwa na viongozi waliopa hivi sasa katika nafasi za ubunge na uwakilishi.
Alieleza kuwa watu wanaofanya hivyo wajue kwamba bado Chama Cha Mapinduzi hakijatangaza mchakato wa uchaguzi hivyo wanachokifanya ni kuvunja kanuni,miongozo ya Chama na sharia za nchi.
Katika maelezo yake Dkt.Dimwa, ameweka wazi msimamo wake kuwa katika uongozi wake atawachukulia hatua kali za kinidhamu watu waotengeneza makundi na safu za kukigawa Chama na kuchonganisha viongozi na wananchi.
“Natumia nafasi hii kukumbusheni kuwa CCM tayari imemaliza uchaguzi wa Chama na kuvunja makundi yote, hivi sasa tuna kundi moja ambalo ni Chama Cha Mapinduzi, na kazi yetu kubwa ni kutatua kero na changamoto za wananchi.”,alisema Dkt.Dimwa.
Kupitia hafla hiyo alimuagiza Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Chumbuni,kuhakikisha anawafikisha katika kamati ya usalama na maadili watu wote watakaobainika kuhusika na migogoro,uchochezi na makundi ya kuhatarisha uhai wa chama jimboni humo.
Dkt.Dimwa, aliwasihi viongozi hao wa majimbo kuwa wajibu hoja kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi walizozitoa wakati wa kampeni zilizopita mwaka 2020.
Alisisitiza kuwa hatua hiyo itarejesha imani kubwa kwa wananchi katika kuiamini CCM kwenye kuleta maendeleo endelevu.
"Ili CCM iendelee kukubalika na kuaminiwa na wananchi kupewa ridhaa yakuongoza Zanzibar kuna umuhimu mkubwa kwa viongozi wa chama kuwa karibu na wananchi kuwatembelea kusikiliza kero zao,"alisema
Alisema CCM inatambua kuwa huduma ya maji safi na salama ni huduma ya msingi ya kila mkazi wa Zanzibar.
Pia,alisema kuwa katika miaka mitano(2020-2025) CCM iliahidi kupitia ilani yake ya uchaguzi ukurasa wa 243 ibara ya 186 vifungu vidogo vya (a)-(i) kwamba inaielekeza SMZ kuendelea kutimiza azma ya ASP na CCM ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wote.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chumbuni, Ussi Salum Pondeza alisema kisima cha mwanzo kilikauka tangu mwaka 2008.
Alisema kisima hicho kiliharibika Aprili mwaka 2022 na kusababisha wakazi wa Jimbo hilo la Chumbuni kuhangaika na kukosa huduma ya maji safi na salama.
"Hivyo kutokana na hali hiyo wakazi wa shehia hizi zilizopo katika Jimbo la Chumbuni walikuwa hawapati huduma za maji hivyo nikatumia nguvu zangu nikawaleta wataalamu tukaanza kuchimba kisima hichi kipya,"alisema
Mbunge huyo alisema kisima hicho kilianza kuchimbwa katika kipindi cha January mwaka huu.
Alisema kisima hicho ambacho kimechimbwa hivi sasa kitahudumia shehia nne ikiwemo Masumbani,Banko,Maruhubi na Karakana ikilinganishwa na kisima cha awali ambacho kilikuwa kinahudumia shehia mbili.
No comments:
Post a Comment