Habari za Punde

Cde.Mbeto: Awafariji Wazee na Waasisi wa CCM wa Wilaya ya Mjini Unguja

Na.IS-HAKA OMAR -ZANZIBAR.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi Khamis Mbeto Khamis, ametoa wito kwa viongozi wa CCM ngazi zote kuendeleza utamaduni wa kuwa karibu na jamii.

Rai hiyo ameitoa leo katika ziara yake ya kutembelea waasisi wa CCM na Wazee wasiojiweza  katika wilaya ya Mjini kichama.

Mbeto,amefafanua kuwa Chama Cha Mapinduzi kina utajiri wa rasilimali watu wakiwemo wazee waliofanya kazi kubwa ya kuasisi Chama kabla na baada ya Afro-shiraz party(ASP) na baadae kuzaliwa CCM iliyorithi misingi imara ya uongozi,uchumi,itikadi,sera na falsafa za maendeleo.

Alisema hakuna kitu chochote cha kuwalipa wazee hao chenye thamani  zaidi ya kufarijiwa na kuwaombea dua  za mara kwa mara ili waendelee kuwa na afya njema.

Alieleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kuwatembelea wazee waasisi na wagonjwa kwa ajili ya kuwajulia hali na kuwapatia futari ikiwa ni kuendeleza utamaduni wa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wa kutembelea makundi hayo.

“Wito wangu kwa viongozi na watendaji wa Chama na Jumuiya zake zote,tuendeleze utamaduni wa kuwatembelea wazee wetu ili kuwafariji kwani wengi wao wanaishi kwa upweke na kujihisi kama wametengwa.

Tuna viongozi kuanzia ngazi za mashina hadi Taifa hivyo kwa Chama na Jumuiya tuwatembelee wazee wetu na ikibidi tuwafanyie na kuwasaidia kazi kama kuwafulia nguo na kufanya usafi wa maeneo wanayoishi.”,. alifafanua Mbeto.

Nao baadhi ya wanafamilia waliotembelewa na Katibu Mbeto, wamekipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kuthamini mchango wao.

Kwa upande Wazee waliotembelewa na Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi Khamis Mbeto ni pamoja na ndugu Kombo Mzee kombo,ndugu Somoe Ali Hassan.

Wengine ni ndugu Tatu Sobo, ndugu  Atte Salum Said,ndugu Thani Simba Tabu,ndugu Mosi Juma Foum pamoja na ndugu Sultan Muhammed Ali ambao wote ni waasisi wa Chama Cha Mapinduzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.