Habari za Punde

Kafulila Aelezea Mkakati wa Kufutia Trilioni 21 ZA PPP


Kamishna wa Idara ya PPP Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. David Kafulila akizungumza wakati akitoa mada kwenye semina elekezi kwa baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari nchini, iliyolenga kuwajengea uelewa wa masuala mbalimbali yanayotekelezwa na Wizara ya Fedha na Mipango, kwenye ukumbi wa Hazina ndogo, jijini Arusha.
Baadhi ya Wahariri wa vyombo vya habari nchini wakifuatilia kwa umakini mada iliyotolewa na Kamishna wa Idara ya PPP Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. David Kafulila (hayumo pichani) kuhusu Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika semina elekezi iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kuhusu masuala mbalimbali yanatokelezwa na Wizara hiyo, katika ofisi ndogo ya Hazina, jijini Arusha.

Na Benny Mwaipaja, Arusha

Serikali inapanga kukutanisha wakuu wa mashirika ya umma 7 ya kimkakati na wabobezi wa uwekezaji wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) mwezi ujao kwa lengo la kubadilishana uzoefu utakaosaidia kuvutia mitaji ya kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 9 (sawa na Sh. trilioni 21) ndani ya miaka mitatu.

 

Kamishna wa Idara ya Ubia kati ya Sekta ya Umma  na Sekta Binafsi (PPP), Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. David Kafulila. alisema kuwa mkutano huo utakaofanyika Mei 2-6 ni sehemu ya mkakati wa kufikia malengo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDPIII).

 

Alisema Mpango huo umeainisha mahitaji ya fedha zitakazotumika kuutekeleza kuwa shilingi trilioni 114 ambapo kati ya fedha hizo, zaidi ya shilingi trilioni 60 zinatakiwa kutoka Serikalini na kiasi kilichobaki cha sh. trilioni 40.3 kinatarajiwa kutoka Sekta Binafsi.

 

“Katika mgawanyo huo, zaidi ya Shilingi trilioni 21, sawa na asilimia 17 ya ugharamiaji wa mpango huo, zinatakiwa kuchangiwa na utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ((PPP), na hilo linahitaji mikakati ya kufikia lengo hilo”alifafanua Bw. Kafulila

 

Akizungumza katika mkutano kati ya Wizara ya Fedha na Mipango na wahariri wa vyombo vya habari nchini uliofanyika Ofisi za Hazina Ndogo ya Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Arusha, Bw. Kafulila alisema kuwa wabobezi hao wa PPP wanatarajiwa kutoka kwenye taasisi ya Benki ya Dunia ya inayojihusisha na utoaji wa mitaji kwa Sekta Binafsi, International Finance Corporation (IFC).

 

Bw. Kafulila alibainisha kuwa warsha hiyo itazishirikisha taasisi  za umma, ikiwemo Shirika la Umeme-TANESCO, Wakala wa Nishati Vijijini-REA, Shirika la Reli Tanzania-TRC, Mamlaka ya Uendelezaji Viwanja vya Ndege-TAA, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania-TPDC, Mradi wa Mabasi ya Mwendokasi Dar es Salaam-DART na Shirika la Bandari Tanzania-TPA, zitabainisha namna zilivyojipanga kutekeleza miradi kwa utaratibu wa PPP ndani ya miaka mitatu.

 

"Serikali imejipanga kutumia fedha kununua utaalamu kuhakikisha miradi ya PPP inaandaliwa kwa weledi mkubwa ili kuvutia mitaji duniani," alisema.

 

Alisisitiza kuwa mpaka sasa kuna miradi minne ya PPP sokoni, na mingine 21 iko katika hatua ya upembuzi.

 

"Miradi ya PPP iliyopo sokoni kwa sasa ni pamoja na mradi wa barabara (Expressway) kuanzia Kibaha- Chalinze,  Mradi wa mabasi yaendayo kasi (BRT), Ujenzi wa hoteli ya nyota 5 katika uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA), pamoja na ujenzi wa eneo la biashara la kimataifa (Business Complex)," alisema.

 

Bw. Kafulila alisisitiza kuwa PPP ni ajenda kubwa ya duniani sasa kwa sababu mahitaji ya wananchi ni makubwa kuliko uwezo wa Serikali kufikia kwa kutumia mikopo na kodi. 

 

Alisisitiza kuwa deni la Taifa kwa Tanzania la takriban asilimia 40% ya uchumi ni kiwango cha wastani na himilivu na kwamba kama nchi inafanya vizuri kulinganisha na nchi zote za Afrika Mashariki na nyingi Kusini mwa Afrika kwa mujibu wa ripoti zote za taasisi ya Moody's. 

 

Hata hivyo, aliongeza kuwa pamoja mwenendo mzuri wa usimamizi wa uchumi na deni,  tafiti zinaonesha kwamba tuendako mahitaji ya miundombinu yatakuwa makubwa na hivyo kuepuka kuumiza wananchi kwa kodi kubwa na mikopo zaidi, ni lazima kutazama PPP kama mbadala nafuu.

 

"Tafiti zinaonesha kuwa miundombinu tuliyonayo Tanzania sasa hivi ambayo tumejenga kwa takriban karne moja, mfano reli ya kati, inatosha theluthi moja tu ya mahitaji ya taifa ya miundombinu ifikapo mwaka 2050," aliongeza.

 

Hivyo kutoka sasa na 2050 tunahitaji kujenga miundombinu mara mbili ya iliyopo sasa, alisema.

 

Baadhi ya Wahariri wa Vyombo vya habari wamepongeza jitihada za Serikali za kuishirikisha kikamilifu sekta binafsi kutekeleza miradi ya Taifa ya kimkakati kwa njia ya PPP kwa kuwa hatua hiyo itaharakisha Maendeleo ya nchi.

 

Walisema kuwa mchango wa Sekta binafsi katika Maendeleo ya nchi mbalimbali duniani unazipunguzia nchi mzigo wa kutumia Bajeti zao kutekeleza miradi hiyo na kuelekeza rasilimali fedha kidogo zinazopatikana kutoka vyanzo vyao vya fedha kwenye miradi mingine ya huduma za jamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.