Habari za Punde

MBETO: Asema CCM Itaishauri Serikali Kuongeza Kiwango cha Pencheni kwa Wazee

Na. Is-haka Omar -- Zanzibar.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi Khamis Mbeto Khamis,amesema Chama Cha Mapinduzi kitaishauri serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza kiwango cha pencheni ya kujikimu kwa wazee wenye umri wa miaka 70 nchini.

Kauli hiyo ameitoa katika mwendelezo wa ziara yake ya kuwafariji na kukagua wagonjwa na wazee wa CCM, kwa lengo la kuwapatia futari itakayowasaidia katika mwezi huu wa Ramadhani huko katika Wilaya ya Amani Kichama.

Alisema kuwa wazee wa Chama Cha Mapinduzi wanatakiwa kuwa na maisha yenye hadhi inayoendana na Chama hicho  kwani ndio waliojitolea na kufanya kazi kubwa ya kihistoria ya  kuasisi serikali zilizopo madarakani inayokumbukwa na kuenziwa na vizazi vya sasa na vijavyo.

Katibu huyo wa Kamati Maalum Mbeto, alifafanua kuwa dhamira na kipaumbele cha CCM ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora hususani watu wenye mahitaji maalum wakiwe wazee ambao wengi wao hawana nguvu za kujihudumia.

“Lengo la ziara hii ni kuwafariji wazee wetu na kuwajulia hali zao   pamoja na kuwapatia futari itakayowasaidia katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani”, alisema Mbeto.

Aidha,alifafanua kwamba msingi wa pensheni kwa wazee wote wa Zanzibar wa kuwapatia kiasi cha shilingi 20,000 kwa kila mwezi ni sera ya hifadhi ya jamii iliyopitishwa mwaka 2014, ukiwa mpango mkuu wa taifa wa dira ya 2020 unaolenga kukuza uchumi na kupunguza umasikini nchini.

Alisema mpango huo unaokadiriwa kutumia zaidi ya shilingi miioni 435 kwa mwezi ambapo ni sawa na shilingi bilioni 5.220 kwa mwaka.

Alisema kuwa ikumbukwe kuwa Zanzibar inaendelea kuvunja rekodi kwa kuwa  nchi ya kwanza Afrika mashariki kuanzisha mpango huo, na ya sita kwa Afrika baada ya Mauritius, Afrika Kusini, Lesotho, Namibia na Botswana.

Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Amani Bi.Veronica Ndaro, amekishukru Chama kwa kuendelea kufanya ziara mbalimbali za kuwafariji wanachama wake hatua inayoongeza upendo na mshikamano baina ya taasisi hiyo na jamii kwa ujumla.

Wakizungumza kwa wakati tofauti baadhi ya wazee hao waliofarijiwa wamekipongeza Chama na kusisitiza kuwa viongozi hao walinde na kutekeleza ibara ya tano ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2022 ya inayoelekeza ushindi wa Chama kwa kila uchaguzi.

Katibu huyo wa Kamati Maalum ya NEC Mbeto, ametoa futari mbalimbali yakiwemo unga wa ngano,mafuta ya kula,tambi,mchele na sukari kwa wa wazee wa Wilaya za Mjini na Amani kichama.

Wazee hao ni pamoja na Haji Ali Haji,Ramadhani Suleiman Nzori,Rehema Mwinyi Aboubakar,Wahida Haji Jecha,Mtumwa Haji Harufu(Bi.Buku), Mohamed Haji Khatib(Chibadi),Msim Hamad Buhet na Omar Seif Omar.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.