Serikali
kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema itaendelea kuhakikisha miradi ya
mazingira katika maeneo mbalimbali nchini inatekelezwa kwa kiwango
kinachotakiwa ili iwanufaishe wananchi na kutatua changamoto za kimazingira.
Pia, imesema itashirikiana
na Wizara nyingine za kisekta kuona namna namna bora ya kuvuna maji ili
kudhibiti mafuriko yanaoyakumbuka maeneo mbalimbali nchini na kusababisha adha
kwa wananchi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu
wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis leo Aprili 19, 2023
bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Serengeti Mhe.
Jeremiah Mrimi.
Katika swali la msingi Mhe. Mrimi alitaka kujua
mpango wa Serikali wa kudhibiti mafuriko katika Mto Mara kwa kuvuna maji yake
kupitia mabwawa na kujenga skimu za umwagiliaji.
Akiendelea kujibu swali hilo Mhe. Khamis
amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais ina utaratibu wa kutembelea na kukagua
miradi inayoratibiwa na Ofisi hiyo na kutoa maelekezo ikamilike kwa wakati na
kwa kiwango.
Amebainisha
kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais tayari imezindua Mpango
Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) ambao umeelezea
mikakati na shughuli endelevu zinazoweza kufanyika ili kuhifadhi mazingira.
“Mheshimiwa Spika, Mto Mara
ni moja ya mito mikubwa na muhimu nchini Tanzania. Hivyo, Serikali kupitia
Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara nyingine za kisekta zitakaa na kuona namna
bora ya kuvuna maji ili kudibiti mafuriko,” amesema.
Mhe. Khamis amefafanua
kuwa Serikali itaimarisha usimamizi wa vyanzo vya maji na kuhakikisha uwepo wa
mtiririko wa uhakika katika mito ikiwemo mito mbalimbali ikiwemo Mara, Kagera,
Ruaha Mkuu, Momba, Lufurio, Wami na Ruvuma.
Aidha, Naibu
Waziri huyo amesema pia Serikali itahamasisha matumizi sanifu kwa watumiaji
wote wa mito hiyo pamoja na kuimarisha viwango vya maji katika vyanzo mbalimbali
vya maji vilivyopo hapa nchini.
Ikumbukwe Mpango
Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) ulizinduliwa Juni 05,
2022 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa
wakati wa kilele cha Siku ya Mazingira Duniani jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment