Habari za Punde

Azma ya SMZ Kuendeleza na Kufikia Hatua Kubwa Zaidi Katika Sekta ya Utalii Kuendelea Kuwa Sekta Mama ya Uchumi wa Zanzibar

 
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema ina azma ya kuendeleza na kufikia hatua kubwa zaidi kuifanya sekta ya utalii kuendelea kuwa sekta mama ya uchumi wa Zanzibar kwa miaka mitatu ijayo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo kwenye mkutano wa wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari, Ikulu, Zanzibar ikiwa ni kawaida yake ya kuzungumza nao kila mwisho wa mwezi.

Dk. Mwinyi alisema sekta ya Utalii Zanzibar, inachangia asilimia 30 pekee ya pato la uchumi wa Zanzibar, ikilinganishwa na sekta nyengine za Maendeleo, kupitia utalii wa Fukwe, Bahari na Mji mkongwe, ambao umeongeza watalii wengi kiasi ya wawekezaji kuendelea kujenga hoteli nyingi kubwa pamoja na nyumba za wageni za kisasa.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliendelea kusisitiza umuhimu wa Zanzibar kuwa na utalii wa kumbi za mikutano na kueleza kuwa ni chachu ya kukuza uchumi wa nchi na kuongeza haraka fursa za biashara  kwa Serikali, taasisi binasi na wananchi wa kawaida, akitolea mfano wa mkutano mkubwa wa Chama cha Menejimenti ya Makatibu Mahsusi (TAPSEA) na Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) uliofanyika Mei 27 mwaka huu maeneo ya Fumba, Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alisema, kupitia mkutano huo, Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya bara na visiwani kutoka sekta za umma walikusanyika pamoja kujadili masuala yao, hali iliyotoa fursa nyingi za uchumi na biashara zikiwemo, nyumba za wageni kupokea wageni wengi, vyombo vya usafiri wakiwemo bodaboda, taxi, na aina nyengine za usafiri, hoteli, wafanyabiashara wa vyakula, matunda na wenyeji wa eneo lililowakutanisha washiriki wa mkutano huo kwa namna moja ama nyengine walinufaika na fursa hizo.

“Ndio maana naendelea kuwasisitiza wananchi wa Kilimani kuangalia kwa upana wa faida za utalii wa mikutano na fursa zake ili wachangamkie fursa hizo zenye nia ya kuleta mabadiliko makubwa ya uchumi na maendeleo” aliweka misisitizo Dk. Mwinyi.

Alisema, ikitoka sekta ya mafuta na gesi kuibuka na kukua ghafla itachukua nafasi ya sekta ya utalii, kwani duniani kote mafuta na gesi ndio seka kiongozi ya uchumi.

Akitoa ufafanuzi kuhusu ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG), aliyodaiwa kuiopokea kwa siri na kutoitangaza kwa umma, Rais Dk. Mwinyi aliwatoa hofu wananchi na kueleza kwa mujibu wa sheria lazima ripoti iwasilishwe mapema Baraza ya Wawakilishi na bahati baraza lililkua limeanza hivyo, kulikuwa na haja ya kuwasilishwa mapema barazani na baadae taratibu nyengine za kuitangaza zitafuata wiki ijayo.

“Wakati ripoti ya CAG inakuja kwangu, kuna utaratibu wa kisheria kwamba Baraza la Wawakilishi likinza ndani ya wiki moja, siku saba, lazima ripoti ya CAG iwe imeshapelekwa na kwa ratiba na safari tulizokuwa nazo tukasema wacha tuipokee, tumkabidhi Waziri husika aiwasilishe Barazani ndani ya kipindi hicho tusije tukavunja utaratibu wa kisheria” Alifafanua Dk. Mwinyi.

Alieleza ni kweli Baraza limeanza, ripoti ilipelekwa na tayari imepangiwa siku ya kusomwa hadharani.

Akitolea ufafanuzi wa baadhi ya maswali aliyoulizwa kwenye mkutano huo kuhusu ripoti ya CAG, yaliyowahusu baadhi ya wasaidizi wake wakimwemo mawaziri na watendaji wengine wa Serikali endapo ripoti hiyo itawakuta na ubadhirifu ndani ya Serikali anayoiongoza, Rais DK. Mwinyi alieleza, kuna njia tatu za kuwachukulia kwanza ni hatua za kuitawala, ambapo Serikali ikimgundua muhusika amehusika na uzembe fulani, kutoka kwenye ripoti ya CAG atatolewa Serikalini.

Lakini pia Rais Dk. Mwinyi alieleza njia nyengine ya jinai ambapo Serikali haihusiki sana, ikitokea mmoja wa wasaidizi wake amekamatwa na ubadhirifu basi moja kwa moja atapelekwa  mahakamani  nakueleza kwamba wapo baadhi yao wana kesi  mahakamani kutokana na kukutwa na ubadhirifu kwenye ripoti ya CAG kwa nyakati zilizopita.

Kuhusu changamoto za ubovu na uchakavu wa barabara nyingi za mjini na vijini, Dk. Mwinyi alieleza Serikali imezamiria kuzifanyia matengenezo makubwa barabara zote kwa kujibu wa viwango vya maeneo.

Alisema barabara za Mjini zitatofautiana na za mashamba kwa viwango na uimara licha ya zote kutarajiwa kuwa kwenye uimara wa hali ya juu lakini zitatofautiana kwa mujibu wa matumizi ya bara bara hizo pamoja na madaraja na barabara za juu.

Nakueeleza kwamba barabara inayoelekea bandari jumuishi ya Mangapwani itakua yakiwango cha hali ya juu zaidi kwa mujibu wa matumizi yake ya shughuli za bandari.

Akizungumzia Ujenzi wa bandari Jumuishi ya Mangapwani, Rais Dk. Mwinyi alieleza lengo la bandari hiyo ni kuhudumia kanda nzima ya Afika Mashariki sio Zanzibar pekee.

Alieleza awali utaratibu wake ulianza mazungumzo na watu wa Oman, kisha Serikali ilizungumza na watu kutoka Abu Dhabi, alieleza majadiliano hayo yanafanywa baina ya timu ya serikali yenye nia ya kupata mkataba utakaokuwa na maslahi ya nchi na bandari itakayojengwa kwa mujibu wa matakwa ya Serikali ambayo lazima yazingatie sehemu za makontena, mafuta, nafaka, mafuta na gesi eneo huru (Free zone na masuala ya kilojistiki)

Aidha, alieleza Serikali inatarajia kuyapandisha hadhi, maeneo ya Mangapwani na Bumbwini kuwa miji mikubwa ya bandari.

Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi pia alitoa ufafanuzi kufuatia safari yake ya kikazi mjini Doha, Qatar aliyoifanya hivi karibuni na kuwaelezea waandishi wa habari kwenye mkutano huo alivyopata fursa kueleza maeneo mbalimbali ya biashara na uwekezaji yanayopatikana Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.