Habari za Punde

Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Ndg. Haji Azungumza na Waandhi wa Habari

NAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Zanzibar, Mussa Haji Mussa, akizungumza na Waandishi wa Habari Zanzibar,juu ya kutoa ufafanuzi wa tuhuma zilizotolewa hivi karibuni na Vijana wa Ngome ya ACT-Wazalendo dhidi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi,mkutano huo umefanyika Afisi Kuu ya UVCCM Zanzibar Gymkana, 17/05/2023.

Ndugu Waandishi wa Habari.

Awali ya yote, tuanze na kumshukru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kufika siku ya leo tukiwa na neema ya uhai na uzima wa afya  uliyotuwezesha kukutana hapa.

Pili natumia fursa hii kwa niaba ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Zanzibar, kuwashukru sana Ndugu zetu Waandishi wa Habari ambao ni wadau wetu muhimu katika kazi hizi za kuhabarisha jamii.

Ndugu Waandishi wa Habari.

Siku ya Jumanne ya tarehe 15/05/2023 Genge la Vijana wanaojiita ngome ya ACT-Wazalendo Zanzibar walitoa waraka wao wa kumshutumu,kumdhihaki na kumchafua kwa kauli zisizofaa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi juu ya Kauli yake ya kuwapatia fursa ya ajira Vijana wetu wa UVCCM waliojitolea kwa muda mrefu ndani ya Chama na  Jumuiya zake.

Ndugu Waandishi wa Habari.

Ikumbukwe kuwa hoja dhaifu za Genge hilo ni za upotoshaji na zenye lengo la kuingiza nchini yetu katika vurugu na machafuko ya kisiasa, jambo ambalo halikubaliki hasa katika kipindi hiki ambacho nchini yetu inaendelea kupiga hatu za kimaendeleo katika Nyanja za Kiuchumi,kijamii na Kisiasa.  

Ndugu Waandishi wa Habari.

Suala la ajira katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar linatawaliwa na sheria ya Utumishi wa Umma Namba 2 ya mwaka 2011,hivyo chini ya sheria hiyo hakuna suala la ubaguzi kwenye ajira pale zinapotangwa  kwani Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 imeweka sifa na vigezo kwa wananchi wanaohitaji ajira hizo bila kujali itikadi za kisiasa,kidini,kikabila na rangi.

Ndugu Waandishi wa Habari.

Natumia Mkutano huu kulishauri genge hilo la Vijana wa ACT wasikubali kutumiwa kwa kulishwa matango pori,kwanza wakasome Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na mabadiliko yake ya 2010 yaliyotoa ridhaa ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (G.N.U) ndipo watakapogundua misingi ya Serikali hii kuwa haikuundwa na mihemko ya kisiasa kutoka kwa viongozi wao au magenge yao.  

Ndugu Waandishi wa Habari.

Msimamo na kauli ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar  Dk.Hussein Mwinyi,unatokana na matakwa ya Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 ibara ya 136 kifungu kidogo cha (C) kinachosema ‘’Kuimarisha upatikanaji wa ajira kwa vijana kwa kuzalisha ajira angalau 300,000 kwenye sekta rasmi na isiyo rasmi ifikapo mwaka 2025’’. Pia tufahamu kuwa Vijana wa CCM wana sifa,vigezo na uwezo wa kitaaluma hivyo wana haki ya kuajiriwa katika sekta yoyote nchini.

Ndugu Waandishi wa Habari.

UVCCM Zanzibar tunallani vikali kauli zote zisizofaa zilizotolewa na genge la Vijana wa ACT-Wazalendo Zanzibar, dhidi ya Makamu Mwenyekiti wetu mpendwa Dk.Mwinyi, ambaye amekuwa akifanya kazi usiku na Mchana kutetea maslahi,haki na fursa mbalimbali za Vijana nchini na Zanzibar kwa ujumla.

Ndugu Waandishi wa Habari.

Tunatumia nafasi hii kuwataka Vijana hao wa ACT, kabla ya kuandamana kwanza wawambie Vijana walioajiriwa Serikalini  waache ajira zao pamoja na viongozi wa ACT-Wazalendo waliomo ndani ya SMZ wajiuzuru ili wawasaidie kuandamana sambamba na kuzirejesha rasilimali na vitendea kazi walivyopewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inayoongozwa na Rais Dk.Hussein Ali Mwinyi,vikiwemo boti za kisasa za uvuvi,fedha za uwezeshaji wananchi kiuchumi na huduma mbalimbali za kijamii katika nyanja za Afya,Elimu na Michezo ambayo Vijana wa ACT-Wazalendo ni wanufaika wakubwa.

Ndugu Waandishi wa Habari.

Kauli hizi za kichochezi na zilizojaa kashfa na utovu wa nidhamu zimekuwa zikitolewa mara kwa mara na Vijana pamoja na Viongozi wandamizi wa ACT-Wazalendo,taswira inayoonyesha namna Chama hiki cha upinzani kinavyowaandaa magenge ya Vijana wasiojielewa wala kuwaheshimu watu waliowazidi umri na maarifa. Sisi UVCCM Zanzibar tupo imara kulinda nchi na viongozi wetu hivyo tupo tayari kwa lolote tunawaonya wasiandamane wala kuleta fujo...kwa heshima na unyenyekevu tunawaomba viongozi wetu endapo genge hilo litaandamana au kufanya vinginevyo watuachie UVCCM tuwadhibiti pia tunawakumbusha kuwa hii ni nchi ya Mapinduzi.  

 Ndugu Waandishi wa Habari.

Mwisho, tunawaomba vijana wenzetu wa UVCCM watulie kwani Zanzibar ipo salama chini ya uongozi imara wa jemedari wetu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi.

Ndugu Mussa Haji Mussa,

Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM,

Zanzibar,

17/05/2023.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.