Habari za Punde

Sweden Yaonesha Nia ya Uwekezaji Kwenye Biashara Nchini

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa pili kushoto), akizungumza jambo wakati wa Mkutano wake na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Macias, uliofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akieleza kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden, wakati wa Mkutano kati yake na Balozi wa nchi hiyo nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Macias, jijini Dodoma.
Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Macias, akiipongeza Serikali kwa juhudi mbalimbali za maendeleo, wakati wa mkutano na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiagana na Balozi wa Sweden nchini Tanzania Mhe. Charlotta Ozaki Macias, baada ya mkutano kati yao uliofanyika jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati) na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Macias, wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania, baada ya mkutano kati yao uliofanyika jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano, WFM, Dodoma)

Na. Peter Haule, WFM, Dodoma

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameishukuru Sweden kwa misaada mbalimbali iliyoweka alama chanya katika maendeleo ya kiuchumi katika sekta ya nishati, elimu na masuala ya demokrasia.

 Amesema hayo jijini Dodoma, wakati wa mkutano wake na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Macias, ulioangazia ushirikiano wa maendeleo kati ya nchi hizo mbili.

Alisema kuwa misaada inayotolewa na nchi hiyo kwa upande wa mazingira, mabadiliko ya tabia nchi, usawa wa kijinsia, elimu na nishati vinaenda sambamba na ajenda ya Taifa ya maendeleo ikiwemo Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025.

“Utakumbuka kabla ya changamoto ya Covid 19 na Vita ya Rusia na Ukraine, uchumi wa Tanzania ulikuwa unakua kwa takribani asilimia saba, ukuaji huo ulitokana na juhudi zilizofanywa na Serikali ya Tanzania na Washirika wa Maendeleo ikiwemo Sweden, hivyo nchi yako imeweka alama katika kuinua maisha ya watanzania”, alisema, Dkt. Nchemba.

Amesema Tanzania katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi baada ya Covid 19 na Vita ya Risia na Ukraine, imechukua hatua kadhaa ikiwemo kutoa ruzuku kwenye mafuta na kwenye sekta kilimo.

Alisema juhudi zinazoendelea kufanywa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hadi mwaka 2027 uchumi wa Tanzania unatarajia kukua kwa asilimia saba.

Kwa upande wake Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Macias aliipongeza Serikali kwa kuchochea ukuaji wa uchumi, akieleza kuwa licha ya kuwepo kwa mabadiliko ya viongozi na Sera lakini bado kumekuwepo na ushirikiano ambao ni imara katika kupunguza umasikini na ujenzi wa miundombinu nchini.

Alisema kuwa nchi yake itaendeleza ushirikiano wa maendeleo hususani kwenye eneo la biashara kati ya nchi hizo mbili kwa kuwa wamefanya utafiti na kugundua kwa kiasi kikubwa mazingira ya kibiashara Tanzania  ni mazuri.

Alisema anauzoefu mkubwa katika masuala ya kibiashara kupitia nchi nyingine kwenye kutumia usafiri wa umma katika kusaidia uchumi hususani katika miji ambayo inamsongamao wa watu na ongezeko la watu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.