Habari za Punde

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. KassimMajaliwa Avipongeza Vilabu vya Yanga na Simba


Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameungana na Watanzania kuipongeza klabu ya Yanga kwa hatua ya nusu fainali waliyofikia katika mashindano ya kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAF).

Waziri Mkuu Majaliwa amesema hayo Mei 11, 2023 Bungeni jijini Dodoma ikiwa ni utaratibu aliojiwekea katika mikutano ya Bunge kila siku ya Alhamisi kupata wasaa wa kujibu maswali ya Wabunge ya papo kwa papo ili kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali.

“Hakika Dar Young Afrika inaendelea kupeperusha vyema bendera ya Tanzania, na niwapongeze sana kwa matokeo ya jana, tunawaombea kwa mchezo wa marudiano kule Afrika Kusini mshinde kwa magoli mengi” amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza kuwa Watanzania wanahamu ya kuona Tanzania inaingia kwenye mashindano hayo ya CAF kwenye ngazi ya fainali.

Aidha, Waziri Mkuu ameipongeza timu ya Simba kwa hatua iliyofika ambapo amesema anaamini wamejifunza kutoka kwa klabu jirani na hatua waliyofika huku akiamini msimu ujao vilabu viwili au zaidi vifanye vizuri zaidi.

Katika msimu wa 2022/2023 timu za Tanzania za Yanga na Simba zimefanya vizuri kwenye mashindano ya Afrika kwa timu ya Yanga hadi sasa ipo hatua ya nusu fainali Kombe la Shirikisho Barani Africa (CAF) na timu ya Simba ikifikia hatua ya robo fainali ya kombe la Klabu Bingwa Afrika.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.