RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Serikali
ya Norway kwa jitihida zake za kuendelea kuiunga mkono Tanznia ikiwemo Zanzibar
kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo.
Dk. Mwinyi ametoa
shukurani hizo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Balozi wa Norway nchini
Tanzania, Elizabeth Jacobsen aliyefika kuaga baada ya kumaliza kipindi chake
cha utumishi nchini.
Rais Dk. Mwinyi
alimueleza Balozi Jacobsen kwamba, Zanzibar imenufaika na fursa nyingi kutoka
Norway zikiwemo sekta za Afya, Umeme na Elimu.
Amesema uhusiano wa
Norway na Tanzania utakumbukwa zaidi kwa kuinufaisha Zanzibar kupitia sekta ya
umeme, hasa wa kutoka Tanga hadi Pemba na Dar es Salaam hadi Zanzibar ambapo
Dk. Mwinyi alieleza, Norway ilitoa mchango mkubwa kuunga mkono juhudi za
serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzaznia
katika kuwafikishia huduma bora wananchi.
“Tunaishukuru Serikali
ya Norway kwa kuendelea kutuunga mkono Tanzania, hasa kwenye sekta za Afya na
umeme, tunashukuru Norway imetuungamkono kwenye sekta ya umeme, ilisaidia
kueneza umeme visiwani Zanzibar” alisifu Rais Dk. Mwinyi.
Aidha, Dk. Mwinyi
alimueleza balozi huyo dhamira ya Zanzibar kutaka kujitegemea kwa umeme wake
wenyewe ili kuwapatia huduma ya uhakika wananchi wa Unguja na Pemba badala ya
kutegemea umeme kutoka Tanzania Bara.
“Kwa hatua tuliofikia
sasa, Zanzibar inataka isimame wenyewe ijitegemee wenyewe umeme wake utakaozalishwa
hapa hapa Zanzibar” alieleza Dk. Mwinyi.
Pia alisifu Rais Dk.
Mwinyi, alisifu ushirikiano ulipo baina ya Norway na Tanzania hasa kwenye nyanja
za afya na elimu na kueleza Serikali ya Norway imetoa mchango mkubwa kwa
Tanzania kwa kuwajengea uwezo Watanzania wengi kupitia vyuo vikuu vya nchi
hiyo.
“Hatunabudi
kuishukuru Serikali ya Norway, kupitia vyuo vikuu vya afya vya huko
vimewajengea uwezo watu wetu kupitia sekta za Umma na binafsi” alisifu Dk.
Mwinyi.
Akizungumza na Rais
Dk. Mwinyi, Balozi Elizabeth ameisifu Tanzania kuendelea kuwa nchi ya amani, yenye
raia wenye upendo, ushirikiano, umoja na utulivu wa kisiasa akieleza kuwa
Tanzania ni kielelezo cha nchi ya mfano barani Afrika na kwengineko duniani
kuwa ni taifa lenye demokrasia kwa kutekeleza na haki za binaadamu na siasa
safi.
Balozi huyo alimuahidi
Rais Dk. Mwinyi, kwamba Serikali ya Norway daima itaendelea kuiungamkono Tanzania
ikiwemo Zanzibar kwenye sekta za Maendeleo.
Alisema Serikali ya
Norway inajivunia uhusiano wa muda mrefu wa diplomasia uliopo baina yake na
Tanzania na kusifu zaidi ya miaka 50 yaushirikiano wao kwenye masuala
mbalimbali iliwemo ushirikiano walionao baina ya vyuo vikuu vya Norway na
Tanzania ni chachu iliyokuza urafiki baina ya watu wa mataifa wawili hayo
kwenye nyanja mbalimbali za jamii na uchumi.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment