Habari za Punde

Wito kwa Tasnia ya Habari Kuitumia Fursa ya Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Miaka 30 ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, iliyofanyika Zanzibar katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo 3-5-2023.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa wito kwa tasnia ya habari kuitumia fursa ya maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kuweka mkazo kwenye uhuru wa kujieleza ndani ya ajenda ya jumla ya haki za binaadamu, kwa kuangazia uhusiano baina ya uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na haki nyengine.

Aidha, aliwaasa waandishi wa habari kushirikisha wahusika wote kwa madhumuni ya kulinda uhuru wa vyombo hivyo, kuimarisha uhuru wa kujieleza, na kuweka mazingatio ya haki za binaadamu kama kitovu cha kufanya maamuzi kwa ngazi za kimataifa, kikanda na kitaifa.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani huko ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip, Kiembe Samaki, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Katika maadhimisho hayo, Rais Dk. Mwinyi pia aliwataka waandishi wa Habari kutimiza ahadi zilizotolewa na kila nchi Mwanachama wa Umoja wa Mataifa ili kuyafikia malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

Pia Dk. Mwinyi aliwataka wadau wa vyombo vya habari kuitumia siku hiyo kuisherehekea kwa kuungana na mashirika yanayotangaza masuala ya mazingira, haki za wanawake, watoto, haki za kiasili, haki za kidijitali, vita dhidi ya ufisadi na mengineyo.

Alisema, maadhimisho hayo ni jukwaa muhimu katika kuibua changamoto za kisera na kuangalia namna bora ya kuboresha mazingira ya kuendesha vyombo vya habari nchini.

Akizungumzia sheria ya Habari, Rais Dk. Mwinyi alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeandaa mswada wa sheria hiyo yenye madhumuni ya kufuta Sheria iliyopo ya Usajili wa Magazeti, Wakala wa Habari na vitabu Sheiria nambari 5 ya mwaka 1988 ambapo marekebisho yake ni sheria nambari 8 ya mwaka 1997 na kutunga Sheria mpya ya Huduma za Habari na Mambo yanayohusiana na hayo.

Dk. Mwinyi alieleza kwamba Mswada huo tayari uko Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na unatarajiwa kutoa sheria nzuri itakayohusiana na masuala ya habari.

Alisema Zanzibar, imekuwa na kasi ya usajili mpya wa vyombo vya habari hasa vya kielektroniki kupitia Tume ya Utangazaji baina yam waka 2020 hadi 2023. Kwa mijibu wa tume hiyo Dk. Mwinyi alieleza jumla ya TV 21 za kawaida na 38 za mitandaoni zimesajiliwa, jumla ya redio 27 zikiwemo za masafa ya FM na za jamii zimesajiliwa.

Aidha, alizungummzia Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, magazeti na majarida 71 yamesajiliwa tangu mwaka 1998 hadi 2023. Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Shirika la Magazeti ya Serikali ni vyombo vya habari vya Serikali ambavyo navyo vimekuwa vikifanya kazi kubwa za kutoa taarifa kwa umma.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Andrew Kundo, aliviasa vyombo vya Habari nchini kufanyakazi kwa kuzingatia, miongozo, kanuni na sheria zilipo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Naye, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, alisema Serikali kupitia Wizara ya Habari itaendelea kushirikiana na wadau wa vyombo vya habari nchini ili kuendelea kuwapasha habari wananchi.

Mkurugenzi kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania, TAMWA, Joyce Shebe, aliomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuharakisha mchakato wa Sheria ya Habari

Jumla ya magazeti 312 yalisajiliwa nchini hadi tarehe 20 Februari, mwaka huu, ambapo baada ya Uhuru wa Tanganyika, kulikuwa na magezeti 10 tu.

Kwamujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hadi mwezi Februari mwaka huu, jumla ya redio 218, televisheni 68, redio za mtandao nane, televisheni za mtandao 391, blog, majukwaa 73 na cable operators 53 zimesajiliwa Tanzania bara, ambapo taarifa za baada ya uhuru zinaonyesha tulikuwa na kituo kimoja tu cha redio cha Tanganyika na hakukuwa na kituo cha televisheni hata kimoja, blogs wala majukwaa ya mtandaoni.

IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.