Habari za Punde

Wasomi Nchini Watakiwa Kufanya Utafti wa Kina wa Kufuatilia na Kutathmini Kitaalamu Miradi ya Maendeleo Inayotekelezwa na Serikali

Na.Is-Haka Omar - ZANZIBAR.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,amewasihi wasomi nchini kufanya utafti wa kina wa kufuatilia na kutathmini kitaalamu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ili wananchi wajue mafanikio hayo.

 

Kauli hiyo ameitoa  katika kongamano la kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi, la kuelekea miaka mitatu ya uongozi wake  lililoandaliwa na Tawi la Seneti ya UVCCM Mkoa wa Kusini Unguja Skuli ya Biashara ya SOB SUZA iliyopo Chwaka.  

 

Alieleza kuwa utafti huo utawasaidia wananchi kuepuka upotoshaji unaofanywa kwa sasa na baadhi ya viongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo kupitia mikutano yao ya hadhara iliyofanyika kisiwani Pemba.

 

Mbeto, alisema Zanzibar imepiga hatua kubwa za kimaendeleo chini ya uongozi wa Dk.Mwinyi,hivyo wanasiasa na viongozi wa upinzani wanatakiwa kuthamini na kuunga mkono juhudi hizo badala ya kubeza na kupuuza juhudi hizo  kwani nao ni miongoni mwa wanufaika wa maendeleo hayo.

 

"Wasomi msikubali kudanganywa fanyeni utafti juu ya kazi kubwa iliyofanywa na Dk.Mwinyi toka aingie madarakani mpaka Sasa, leteni majibu na kuibua hoja makini za kujenga mshikamano na maridhiano ya kisiasa yanayohimiza ukuaji wa uchumi wa nchi.

 

Wapinzani  tunajua hawawezi kumpongeza wala kusifu juhudi hizo lakini japo mthamini na kuheshimu mamlaka za kiutawala,kwani nanyi ni wananufaika juu ya maendeleo hayo kwani ruzuku,mishahara na huduma zote muhimu za kibinadamu zinazofanywa na Serikali nanyi mnapata kama wananchi wengine",alisema Mbeto.

 

Pamoja na hayo Dk.Mwinyi, aliwasihi vijana hao wa idara ya UVCCM ya  Vyuo na Vikuu nchini kusoma kwa bidii ili wawe wazalendo wa kweli na waelekeze nguvu zao kusomea fani zinazoendana na mahitaji ya soko la ajira nchini zikiwemo za masuala ya Uchumi wa buluu zilizobeba utalii,mafuta na  gesi.

 

Mbeto,alieleza kwamba Serikali ya awamu ya nane chini ya Uongozi wa Dk.Hussein Ali Mwinyi, inatekeleza kwa ufanisi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 katika sekta mbalimbali nchini.

 

Alisema kuelekea miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dk.Mwinyi, tayari amejenga skuli za kisasa kuanzia ngazi za msingi hadi Vyuo Vikuu ili vijana wasome katika mazingira rafiki yanayoendana na mahitaji ya kitaaluma.

 

Alisema katika kuimarisha Uchumi wa nchi serikali imefungua milango ya uwekezaji kwa kusajili miradi mbalimbali ya maendeleo itakayojenga mahoteli makubwa ya kitalii.

 

Alisema serikali imeimarisha sekta mbalimbali zikiwemo miundombinu,afya,elimu,sekta ya anga,nchi kavu na baharini,utalii,uwezeshaji Wananchi kiuchumi,Ustawi wa jamii na kuweka Mazingira rafiki katika Uchumi wa blue.

 

Katibu huyo wa Kamati Maalum ya NEC Mbeto, aliwasihi wananchi wasikubali kupotoshwa kwani nchi ipo salama na inapiga hatua kubwa katika nyanja za  kiuchumi,kijamii,kisiasa,kiutamaduni na michezo.

 

Alifafanua kuwa kasi ya utendaji wa Serikali hiyo ya awamu ya nane imekuwa ni tishio kwa vyama vya upinzani nchini  hali inayosababisha waanze kuchanganyikiwa na kutoa hoja dhaifu.

 

Kupitia kongamano hilo Mbeto,alihoji kauli za baadhi ya wanasiasa wa upinzani Zanzibar wanaodai eti bora miaka zaidi ya 104 ya utawala wa Kisultani na Ukoloni kuliko miaka 60 ya kujitawala wenyewe na kwamba kauli hizo ni za watu wasiokuwa na uzalendo na wanaotakiwa kupuuzwa.

 

Alisema Zanzibar imeendelea kuwa na hadhi na heshima kubwa Kimataifa kutokana na ukuaji wa demokrasia na diplomasia za kimataifa zinazotoa fursa pana kwa nchi zilizoendelea kuja kuwekeza nchini.

 

Katika risala ya Seneti ya Skuli ya Biashara Chwaka tawi la UVCCM SUZA,wamesema wanampongeza Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi kwa kazi kubwa aliyofanya katika sekta ya Elimu na uwezeshaji wa Vijana.

 

Walisema kuwa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fedha,ukosefu wa kadi za jumuiya ya UVCCM na ukosefu wa ofisi ya kufanyika kazi zao za kisiasa za tawi hilo.

 

Kupitia risala hiyo waliahidi kuendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali ya hamasa na kujitolea katika harakati mbalimbali za kulinda maslahi ya Chama na Jumuiya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.