Mwandishi wa Habari Zanzibar Cable Malik Shaharani akiuliza maswali kuhusiana na maadhimisho ya Wiki ya msaada wa kisheria wakati wa mkutano wa Waandishi wa Habari uliofanyika Wizara ya Katiba na Saheria Mazizini Zanzibar,julai 15,2023.PICHA NA FAUZIA MUSSA MAELEZO ZANZIBARNa Rahma Khamis Maelezo
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuandaa mazingira rafiki kwa watoa misaada ya kisheria ili wananchi wapate fursa za kutetea haki zao.
Ameyasema hayo huko Ofisini kwake Mazizini wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria.
Amesema Msaada wa Sheria ni huduma muhimu inayotolewa kwa wanyonge ambao wanadhulumiwa na kukosa fursa za kutetea haki zao katika jamii.
Amefahamisha kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuwasaidia wanyonge kuweza kupata haki zao kwani wengi wao wanaokosa haki hizo ni kutokana na kutokua na uelewa wa sheria hasa maeneo ya vijijini .
“Maafisa wa msaada wa kisheria wanakumbana na changamoto nyingi katika kuhakikisha jamii inaondokana na uonevu,dhulma na utowaji wa rushwa wakati wa kupambania haki zao hivyo tutawapatia mafunzo ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa”, ameeleza Waziri Haroun .
Waziri huyo ameeleza kuwa zaidi ya asilimia 50 katika jamii wamefanikiwa kutatuliwa changamoto zao kupitia maafisa wa Msaada wa Kisheria.
Nae Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Sheria Hanifa Abdalla Said amesema kuwa maadhimisho hayo ni ya nne tangu kuanzishwa kwake ambapo mwaka huu shamra shamra mbalimbali zitafanyika kuelekea kilele cha maadhimisho hayo.
alifafanua kuwa siku ya tarehe 18 wanatarajia kufanya mhadhara wa Msaada wa Kisheria katika Wizara ya katiba na sheria,tarehe 19 kutafanyika bonanza la Mpira wa miguu, mbio za gunia , pamoja na kufukuza kuku,na 20 kutakuwa na usafi ambao utafanyika asubuhi katika fukwe wa kizingo hivyo aliwaomba wananchi kushiriki katika usafi huo .
Aliongeza kwa kusema kuwa katika kilele cha maadhimisho hayo tunzo na zawadi mbalimbali zitatolewa kwa Wasaidizi wa Sheria waliofanya vizuri katika kazi zao.
Kwa upande wake Afisa Mipango Mwandamizi wa LSF, Alphonce Marandu Guru amefahamisha kuwa wiki hiyo ni muhimu kwa wale wanaotoa huduma za kisheria kwani lengo ni kutoa elimu kuhusu shuhuli zao mbalimbali wanazozifanya katika jamii na kuwasisitiza wananchi na Taasisi nyengine kujitokeza kwa wingi ili kuona kwa namna gani maafisa wa msaada wa kisheria wanafanya kazi zao.
Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa kisheria yanatarajiwa kufanyika tarehe 22 mwezi huu katika Ukumbi wa Sheikh Idriss-Abdul Wakil Kikwajuni ambapo Kaulimbiu ni "Mazingira Wezeshi kwa Watoa Msaada wa kisheria ni Daraja la Haki ".
No comments:
Post a Comment