MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman , (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi mteule wa Tanzania nchini Uturuki Balozi Idd Seif Bakari, baada ya kumaliza mazungunzo yao wakati balozi huyo alipofika ofisini kwa makamu leo tarehe 10 Julai, 2023 kumuaga ili kuelekea kituo chake cha kazi.
(
picha na ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar.)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amemtaka Balozi Mteule wa Tanzania nchini Uturuki kwenda kuimarisha mawasiliano na kutekeleza ipasavyo sera ya Diplomaisia ya Uchumi kuishawishi nchi hiyo kuanzisha Kituo rasmi cha kuunganisha shughuli za wafanyabishara na biashara Tanzania.
Mhe. Othman ameyasema hayo Ofisini kwake Migombani mjini
Zanzibar, alipokutana na kufanya mazungunzo na Balozi Mteule wa Tanzania nchini
Uturuki , Balozi Iddi Seif Bakari aliyefika Ofisini kwa Makamu kumuaga
akielekea kituo chake cha kazi baada ya kuteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Amesema kwamba kituo hicho iwapo kitafanikiwa kuanzishwa pia
kinaweza kuongeza wigo wake kwa kufanya shughuli zake sio tu kwa Tanzania,
lakini pia kikafaidisha Kanda yote ya
Afrika Mashariki kwa jumla jambo
litakalosaidia juhudi za nchi za kuendeleza uchumi na kuimarisha maendeleo.
Mhe. Makamu amesema kwamba nchi ya Uturuki imepiga hatua
kubwa za kimaendeleo hivi sasa kwa hivyo
ni muhimu kutumia fursa iliyopo ya mashirikiano katika nyanja mbali mbali za viwanda na
biashara, elimu na maendeleo ya
kijamii kupitia uhusiano ulipo ili nchi iweze
kunufaika na kuweza kupiga hatua.
Aidha Mhe. Makamu amemtaka balozi huyo kutumia uzoefu wake
alioupata katika nchi nyengine ili wafanyabiashara wa Tanzania kufanya shughuli
zao kwa kutumia mfumo na mtindo wa kisasa unaozingatia maendeleo ya Sayansi na
Teknolojia kuchapuza kasi ya maendeleo ya Taifa.
Kwa upande mwengine Mhe.Othman amemueleza balozi huyo kwamba
pia kuangalia , kuchambua na kuainisha
vipaji na taaluma waliyonayo watanzania wanaoishi Uturuki ili waweze kusaidia
nchi yao katika nyanja mbali mbali kama zinavyofanya baadhi ya nchi nyengine
duniani .
Amesema kwamba ni dhahiri kwamba wapo watanzania wengi wanaoishi katika
nchi hiyo ambao wana vipaji vingi,
elimu, ujuzi na maarifa makubwa wanayoweza pia kuyatumia kuyaleta
nyumbani kusaidia nchi yao iwapo wanaunganishwa na kuratibiwa vyema kupitia
balozi za nchi wanazoishi.
Naye Balozi Mteule wa Tanzania nchini Uturuki Balozi Idd Seif
Bakari, amemueleza Mhe. Makamu kwamba atafanya kila juhudi kuitangaza Tanzania
hasa katika sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kufanya ushaiwishi wa kutumia
shirika la Ndege la Uturuki kuitangaza Tanzania hasa Zanzibar kiutalii kupitia
safari zao za ndege za kila siku.
Aidha Balozi Idd amesema katika kuendesha biashara ya utalii
kuna haja ya Tanzania hasa Zanzibar kuiga mifumo ya uendeshaji bishara
kutoka nchi nyengine kwa kupanga na kutenga maeneo maalumu ya biashara
hiyo kuepuka mtindo wa kufanya kila eneo nchini kuwa ni la utalii.
Hata hivyo, amesema kwamba suala la kuitangaza nchi kiutalii
hasa Zanzibar litakuwa nikipaumbele chake hasa kwa kuzingatia kwamba nchi
anayokwenda kuiwakilisha Tanzania inafanya vizuri na kudiriki kukusanya hadi
dola bilioni 16 kwa mwaka zinazotokana na utalii jambo ambalo ni muhimu kutumia uzoefu wao kusaidia Zanzibar.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
10 Julai , 2023.
No comments:
Post a Comment