Habari za Punde

Mkurugenzi afanya ziara ya kushtukiza Nyumba za Wazee Welezo

 Na Maulid Yussuf WMJJWW 


Mkurugenzi Idara ya Uendeshaji na Utumishi Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto bwana Salum Khamis Rashid amefanya ziara ya kushtukiza katika Makao ya wazee Welezo.

Amesema lengo ni kuona hali ya mazingira ya wazee pamoja na mahudhirio halisi ya wafanyakazi  wa hapo pamoja na kuona kuwa kuna  udhibiti mzuri wa wazee ukizingatia hakuna uzio katika eneo hilo.

Amesema Wizara inatambua changamoto zilizopo na inajitahid kuona namna gani inayatatua matatizo hayo ikiwemo tatizo la uzio ili kuwaweka mazingira mazuri wazee pamoja na wafanyakazi wake.

Aidha amewataka kutimiza majukumu yao kwa kuisaidia Serikali kutimiza malengo yake yakiwemo kutoa huduma bora kwa wazee.

Pia amewataka kuwa wavumilivu kwa kuwasaidia wazee na kuwatunza kwa hali yeyote na kuona kuwa, ikiwa uhai upo nao watakuwa wazee na watahitaji kushughulikiwa.

Amewataka kuwa na  uvumilivu, pamoja na kutambua kuwa kazi yao ni kuitumikia jamii, hivyo kuishi kwao vizuri na wazee hao kutawapa baraka zaidi katika maisha yao.

Hata hivyo amewataka kufanya kazi kwa mashirikiano na upendo wa hali ya juu kati yao na wazee, bila ya kujali ugumu wa kazi.

Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto bwana Abeid Said Muhram, amewashauri wasimamizi wa wazee wanapofanya maombi ya mahitaji yao kuomba kwa miezi mitatu mitatu ili kupunguza tatizo la ukosefu wa vitu wanapoomba kila mwezi.

Nae Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Wazee wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto bi Kame Sheha Ussi ameiomba Wizara   wanapopeleka maombi ya mahitaji ya vifaa kwa ajili ya wazee  kuyafanyia uharaka, kwani huduma zote za wazee zinahitaji vifaa pamoja na dawa za kusafishia ili kuweka mazingira mazuri na salama kwa wazee.

Kwa upande wao  wafanyakazi hao wameomba kupimwa afya zao kila baada ya miezi mitatu, kwani huduma wanazozitoa ni ngumu.

Hata hivyo wamesema  bado kuna changamoto za upatikanaji wa dawa hasa za maradhi makubwa ya wazee pamoja na tatizo la uzio katika eneo lao kwani vitendo vya uhalifu vimekuwa vikifanyika na kupelekea kujeruhiwa baadhi ya wafanyakazi na kuibiwa kwa wazee.

Mpaka sasa Makao ya Wazee Welezo kuna  jumla ya wazee 36 wakiwemo 24 wanaume na 12  wanawake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.