21 Julai, 2023
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amehimiza
jamii kufanya utafiti kwenye nyanja mbalimbali ili kutanua wigo na kukuza elimu
kupitia sekta za maendeleo.
Al hajj Dk. Mwinyi alitoa nasaha hizo kwenye Masjid
Abuu Ubayda, Fuoni Meli Saba, Mkoa wa Mjini Magharibi, alikojumuika na waumini
wa dini ya Kiislamu kwenye ibada ya sala ya Ijumaa.
Alisema,
mataifa makubwa yaliyoendelea yamewekeza mtaji mkubwa kwenye elimu, ambao hutumia
fedha nyingi kushajihisha elimu.
Al
hajj Mwinyi alieleza kadri ya mataifa hayo yanavyotumia pesa nyingi kwenye
elimu, ndivyo wanavyopiga hatua zaidi za maendeleo.
“Ukisikia
kuna nchi inafanya maendeleo makubwa basi ujue ndani yake watu wamejikita mno katika
masuala mazima ya elimu, suala la Utafiti maana elimu inaletwa na utafiti”
Alisema,
elimu ndio inayoleta mabadiliko makubwa kwenye jamii maendeleo yote yanatokana
na elimu watu kujifunza elimu ya dini na dunia.
Kwaupande
mwengine Al hajj Dk. Mwinyi alieleza elimu ya dini huwapandisha darja waumini
wake kwa kuendelea kumcha Mwenyezi Mungu kikweli katika kutekeleza ibada ya
haki kama inavyotakiwa.
Pia,
Alhaj, Dk. Mwinyi amewasihi wazazi/ walezi kuendelea kuwahimiza watoto wao
kusoma elimu zote mbili ya dini na dunia, ili kukuza taifa lenye vijana
wenye maadili na busara ya kukimbilia maendeleo kwa ajili ya familia zao na
taifa kwa ujumla.
Alieleza,
miongoni mwa sababu zinazochangia mmong’onyoko wa maadili kwenye jamii ni
ukosefu wa elimu zote mbili, hivyo aliiasa jamii kuweka mkazo zaidi kwenye
elimu na kulinda maadili ya uislamu.
Hata hivyo, Al hajj Dk. Mwinyi aliitaka jamii
kuendelea kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu kwa kufuata mafundisho ya Mtume
(SAW) kwa kufanya yaliyo mema na kuacha mabaya yanayomchukiza Allah (S.W).
Naye, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi
ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, ameisisitiza jamii ya waislam kuendelea kukithirisha ibada hasa kwenye mwezi
mtukufu wa Muharram.
Alisema, Mwezi wa Mfunguo
nne (Muharami) ni miongoni mwa miezi mitukufu ya Mwenyezi Mungu baada ya
Ramadhan. Pia alisisitiza mwezi 10 Muharam ni Sunna kufunga kwa waumini wa dini
ya kiislam, funga ya Ashura, aliyoieleza
ni funga bora baada ya Ramadhani ambayo Mtume (SAW) aliifunga mara baada ya
kuhamia Madina.
Naye, Khatibu wa sala hiyo ya Ijumaa, Sheikh
Sultan Nassor, aliwahimiza waislam kuendelea kuwa wachamungu kwa kumcha Allah
(S.W) kwa haki ili kujiepusha na yote aliyoyakataza.
Akizungumza kwenye msikiti huo wa Abuu Ubayda,
Fuoni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mahad Istiqama, Sheikh Said Khalfan aliisihi
jamiii kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Muft katika kutatua changamoto zao.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment