Naibu
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe akisaini kitabu cha
wageni muda mfupi baada ya kuwasili katika Banda la Ofisi ya Makamu wa
Rais inayoshiriki Maadhimisho ya Sikukuku ya Wakulima Duniani (Nanenane)
yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya jana
Jumamosi (Agosti 5, 2023). Anayeshuhudia ni Msaidizi wa Mtendaji Mkuu
Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Habiba Mhina.
Naibu
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe akizungumza jambo na
Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais wakati alipotembelea Banda la Ofisi
hiyo inayoshiriki Maadhimisho ya
Sikukuku ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayofanyika Kitaifa katika
Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya jana Jumamosi (Agosti 5, 2023).
Kulia ni Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Zanipha
Msangi.
Naibu Waziri wa
Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa
kuandaa Kitabu cha Muungano ambacho kitasaidia kutoa elimu kwa wanafunzi wa
shule za msingi na sekondari kufahamu chimbuko, historia na mafanikio ya
Muungano huo.
Mhe. Kigahe ametoa
pongezi hizo leo Jumamosi (Agosti 5, 2023) wakati alipotembelea Banda la Ofisi
ya Makamu wa Rais inayoshiriki katika maonesho ya Sikukuu ya Wakulima
(Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.
Mhe. Kigahe amesema
Muungano ni tunu ya taifa ambao umeendelea kudumu kutokana na misingi ya imani,
amani, umakini na usikivu wa Viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hatua iliyowezesha kupatikana kwa
mafanikio makubwa baina ya wananchi wa pande zote mbili.
Aidha Naibu Waziri
Kigahe ametoa wito kwa wananchi na viongozi kutimiza wajibu wa kuuenzi,
kuudumisha, kuuimarisha na kuuendeleza Muungano kwa faida ya vizazi vya sasa na
vijavyo kwa kutoa elimu kwa vijana inayohusu historia, msingi na chimbuko la
Muungano.
Kwa mujibu wa
Mhe.Kigahe amesema Kitabu cha Muungano pindi kitakapoanza kufundishwa mashuleni
kitakuwa nyenzo muhimu ya msingi wa maarifa na taarifa sahihi kwa wanafunzi
kufahamu historia na mafanikio yaliyopatikana katika Muungano.
Naipongeza Ofisi ya
Makamu wa Rais kwa kuandaa kitabu hiki ambacho kimekuja kwa wakati mwafaka
kwani kitawezesha vijana wetu kuweza kujifunza na kuelewa kwa mapana historia
ya Muungano wetu ambao umeleta mafanikio lukuki kwa wananchi wa pande zote
mbili” amesema Mhe. Kigahe.
Kwa upande wake, Afisa
Maendeleo ya Jamii Mkuu, Idara ya Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais alimshukuru
Naibu Waziri Kihage kutembelea Banda la Ofisi hiyo kwani kupitia maonesho hayo
elimu ya masuala ya Muungano na Mazingira imeendelea kutolewa kwa wananchi na
wadau mbalimbali kwa ajili ya kukuza uelewa wa pamoja.
Katika hatua nyingine,
Naibu Waziri Kigahe amepongeza hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na
Ofisi ya Makamu wa Rais katika kuhamasisha juhudi za utunzaji na uhifadhi
wa mazingira kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191.
Ofisi ya Makamu wa
Rais imeungana na Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za umma na binafsi
kushiriki Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane)
yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya
yanayoongozwa na kauli mbiu isemayo “Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa
Mifumo Endelevu ya Chakula”
No comments:
Post a Comment