RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ametoa wito kwa Wahandisi wanawake kushirikiana na kuhakikisha wanachangia vilivyo maendeleo ya nchi kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa juu, wa kati ifikapo mwaka 2025.
Dk. Mwinyi alitoa wito huo kwenye ufunguzi wa Kongamano la nane
la Wahandisi wanawake, ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini
Magharibi.
Alisema, Serikali za
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar, zinatambua na kuthamini
mchango wa Wahandisi wanawake nchini kutokana na kazi za uhandisi
wanazozifanya.
Alisema, Makangamano kama hayo yamekuwa na mchango
mkubwa wa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuendeleza ubunifu wa sanyansi na
kuleta chachu ya maendeleo ya Taifa ikiwemo ujenzi wa viwanda.
Dk. Mwinyi aliongeza, Serikali zote mbili zinajitahidi
kushirikisha wanawake kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kuwawekea
mazingira wezeshi ya kujiajiri, kuhamasisha utambuzi wa fursa mbalimbali kupitia
rasilimali zilizopo nchini, kurejesha stadi za ujuzi, elimu ya uanagenzi vyuoni
na kutenga bajeti kwa ajili ya kufanikisha shughuli za utafiti na ubunifu wa
fani tofauti.
Alisema, fani ya uhandisi ina umuhimu mkubwa kwa
ustawi wa nchi pia ni uti wa mgongo wa shughuli nyingi za kiuchumi. Hivyo
aliwataka vijana na wanawake kuzitumia fursa ziliopo ili kuyafikia malengo yao.
Pia, aliwashauri wahandisi wanawake kufungua kampuni
na kujiajiri kupitia ukandarasi na uhandisi nakueleza hatua hiyo itachangia sana
maendeleo ya nchi kwa kujenga miundombinu imara itakayodumu kwa muda
uliokusudiwa.
Aidha, alieleza kutokana na idadi ndogo ya
wahandisi iliopo nchini, Serikali za SMZ na SMT zinaendelea kuweka mipango madhubuti
ya kuongeza idadi ya wahandisi wanawake na mafundi sanifu pamoja na kuhakikisha
wanasaidiwa vizuri wasichana wanaosoma masomo ya Sayansi katika elimu za
Sekondari, vyuo vya mafunzo ya amali na vyuo vikuu, hatua ambayo bila shaka
itasaidia kuongeza idadi ya wahandisi wanawake nchini.
Hata hivyo, alihimiza ushirikiano baina ya
wahandisi wanawake wa Zanzibar na Kitengo cha Taasisi ya Wahandisi Tanzania
Bara kwa madhumuni ya kuendeleza sekta ya uhandisi nchini Tanzania.
Akizungumza kwenye kongamano hilo kwa niaba ya
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Makame
Mnyaa Mbarawa, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Mhandisi Aisha Amour
alisema Serikali inatambua mchango wa wahandisi katika
kukuza uchumi wa taifa uanzishwaji wa
viwanda mbalimbali.
Naye,
Waziri wa Ujenzi,
Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Muhamed alieleza
kongamano la nane la wahandisi wanawake linaloendelea visiwani Zanzibar
litaongeza hamasa na uelewa kwa vijana na kuwashajihisha zaidi wanafunzi
kuendelea kupenda masomo ya sayansi ili kujijengea kada zenye tija na utaalamu,
kwani bado mahitaji ya wahandisi wanawake bara na Zanzibar yanahitajika.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa taasisi ya wahandisi Tanzania, kitengo cha wanawake,
Rihanna Juma aliisihi jamii kuachana na mitazamo potofu juu ya wahandisi
wanawake kwa kuangalia mapungufu yao yanayotokana maumbile ya jinsia zao
zikiwemo uzazi na uhalisia wao, hivyo aliwataka waajiri kuona umuhimu wao na
kutambua mchango wao kwa maendeleo ya taifa kwa kuwatumia kwenye kazi za
vitendo badala ya kuwapa kazi za ofisini pekee.
Uzinduzi wa Kongamano la nane la wanahandisi wanawake Tanzania kwa mwaka
huu, 2023 ulikwenda sambamba kaulimbiu isemayo “Nguvu ya Ushirikishwaji na Uhusishwaji wa
Wanawake katika kazi za Kihandisi”
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU-ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment