Na Mwandishi Wetu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb), ameliagiza Jeshi la Polisi kutumia sheria na taratibu zilizopo kudhibiti mtu yeyoye mwenye viashiria au lengo la kuvuruga amani hapa nchini.
Mhe. Sagini ametoa maagizo hayo alipotembelea na kukagua Kituo kidogo cha Polisi Bwanga Wilayani Chato katika Mkoa wa Geita ambapo alipokelewa na Mwenyeji wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita ACP Safia Jongo.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na sisi wasaidizi wake hatutomvumilia mtu yeyote mwenye lengo la kuvuruga amani na usalama wa nchi yetu tutamshughulikia vilivyo bila kujali ni nani,” Amesema Sagini.
Naibu Waziri Sagini amelipongeza Jeshi la Polisi Mkoani Geita kwa kufanikiwa kudhibiti vurugu zilizoanzishwa na vijana dhidi ya Jeshi hilo kufuatia kuingilia kati kuokoa maisha ya raia aliyekuwa anashambuliwa na Wananchi kwa kutuhumiwa kuiba vifaa vya mziki msibani katika eneo la Bwanga Mkoani humo.
Pia ametoa rai kwa Wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwa kudhuru maisha ya wenzao kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai na kuwataka kuimarisha shughuli za polisi jamii kwa lengo la kuimarisha usalama, kudhibiti uhalifu na kuepuka kujichukulia sheria mkononi.
Aidha amemtaka Kamanda wa Polisi na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama Mkoani humo kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu na mali zao.
Naye, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita ACP Safia Jongo, amemshukuru Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kufika kituoni hapo huku akimuhakikishia kuwa hali ya usalama mkoani humo ni shwari na wale wote wenye kuleta viashiria vya uvunjifu wa amani watashughulikiwa.
No comments:
Post a Comment