Habari za Punde

Sekta ya Bima Yapongezwa kwa Kuwa Mchango Mkubwa katika Pato la Serikali

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akimkabidhi TUZO Meneja wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) Ndg.Sabri Omar Ali,wakati wa hafla ya Siku ya Bima Tanzania iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar  na (kushoto kwa Makamu) Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo A. Saqware na Rais wa Taasisi ya Bima Tanzania (IT) Bi. Magreth Ikongo. 
Maofisa wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) wakiwa na Afisa wa Wizara ya Fedha ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na TUZO yao baada ya kukabidhiwa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Bima Tanzania yaliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Jijini Zanzibar.

Tumeshiriki katika kongamano la Siku ya Bima Nchini lililoandaliwa na Taasisi ya Bima Tanzania katika Hoteli ya Verde iliyopo Mtoni, Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo Mgeni Rasmi katika shughuli hiyo  alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Kongamano hilo pia lilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wa chama na Serikali, wakiwemo Katibu mkuu kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, Mhe. Japhet Hasunga, Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao pia ni Mabalozi wa Bima.

Akiwakaribisha wageni waalikwa, Rais wa Taasisi ya Bima Tanzania (IT) Bi. Magreth Ikongo, alieleza mchakato mzima wa Maandalizi ya Kongamano hilo ambalo lilianza na zoezi la kukabidhi vifaa mbalimbali vya kiafya katika Hospitali ya Mwananyamala Jijini Dares salaam, pamoja na kukabidhi Kompyuta 10 katika shule ya Sekondari Mikindani iliyopo Dole Mjini Magharibi Zanzibar, pamoja na Matembezi ya Bima valiyofanyika Jijini Dares Salaam.

Kwa upande wake Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo A. Saqware alieleza mipango mbalimbali ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania kwa kushirikiana na Serikali kama vile, Kuandaa Skimu ya bima ya Kilimo, Bima ya Afya kwa wote, Mpango wa kukatia Bima vyombo vya Serikali, kutoa miongozo mbalimbali inavosimamia haki ya mkatabima.

Wakati wa Hotuba yake, Mgeni Rasmi ambaye ni Makamu wa Rais wa pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla aliipongeza Sekta ya bima kwa kuwa na Mchango mkubwa katika kuongeza pato la serikali lakini pia alipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi nyingine kama vile UDSM, PSSSF, IFM, SUZA, IFM na Taasisi nyingine kwa kuanza mchakato wa kuanzisha Bodi va Wataalam wa Bima Hifadhi va jamii na Watakwimu bima (Insurance Social protection and Acturial Board). 

Aidha, wakati akihitimisha hotuba yake, Mgeni rasmi alikubaliana na Ombi la Naibu Kamishna wa Bima la kutaka magari yote yanapopata leseni, yakatiwe bima kabla hayajaingia Barabarani, hii itasaidia kwa baadhi ya wamiliki wa magari ambao wanakwepa Bima, kukatia Bima vyombo vyao kwa usalama wao, vyombo vyao pamoja na watumiaji wengine wa njia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.