Habari za Punde

Tupambane kuzikabili athari za kimazingira - Mhe Othman






Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema kila mmoja ni muhusika katika Vita dhidi ya tishio la mazingira, kutokana na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi, hapa Visiwani na Duniani kote.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo wakati wa Ziara yake katika maeneo ya Mtopepo na Donge Muwanda, Wilaya za Kaskazini A na Magharib A Unguja, kuona na kukagua tishio la mazingira kwa maisha na makaazi ya wananchi.
Amesema kwa sasa tatizo la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ni wajibu wa kila mtu, ili kuiokoa Nchi, Taifa na Dunia yote, ibaki salama.
Mheshimiwa Othman amefahamisha kwamba Serikali, Wananchi na Mamlaka zote, wakiwemo wataalamu, wanahitaji kutumia kila busara kuona mazingira yanabaki salama, licha ya Nchi kufungua fursa za uwekezaji nawimbi la miradi ya maendeleo.
"Nchi yetu watu wengi wanapenda kuja kuwekeza, bali lazima sisi kama Serikali tuone namna gani ya kuiendesha miradi hiyo ili kuyanusuru mazingira", amesisitiza Mheshimiwa Othman.
Aidha Mheshimiwa Othman ameongeza kwakusema, "kiwango gani cha mchanga kitoke nje ya Nchi; Miradi ya aina gani na kila hali, hiyo ni kazi ya Wataalamu wetu ambao hawajawezeshwa kutumia utaalamu wao ili kuilinda Ardhi ya Nchi hii".
Akiweka msisitizo baada ya kukagua eneo la machimbo huko Donge Muwanda, na hususan shimo ambalo watoto wanne (4) walipoteza maisha mapema Mwaka huu, baada ya kutumbukia ndani yake, Mheshimiwa Othman amekaririwa akisema, "kunahitajika njia rasmi ya kudhibiti pamoja na mfumo sahihi wa kuchimba mchanga hapa Nchini".
Kabla ya hapo, Mheshimiwa Othman ametoa Miongozo na Maagizo ya kuwaita Wahusika wote sambamba na Watendaji katika Maeneo na Mamlaka husika, kuja nakuketi ili kutafakari namna bora ya kukabiliana na changamoto zilizojitokeza, na pia namna bora ya kuinusuru Nchi kutokana na tishio la mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Pamoja na miongozo hiyo, Mheshimiwa Othman ameeleza kuitikia kilio cha wananchi katika kuangalia busara na mbinu mbadala katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuzingatia sababu kujipatia rizki za halali, huku akiahidi kuyachukua mapendekezo yao ili kuyafanyia kazi, na hatimaye kuja na mrejesho wa kitaalamu wa namna ya kuyatunza na kuyatumia maeneo yaliyopatwa na athari za kimazingira, yatumike kwa maslahi ya jamii na maendeleo ya Nchi.
"Tumeamua tuitumie hii ili iwe fursa kukaa na kushauriana na kisha tupate mrejesho wa kitaalamu badala ya kuwa tunasema tu bila kupata suluhisho ikawa tunaweka 'museum' (makumbumbusho) ya tatizo", amesema Mheshimiwa Othman.
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Harusi Said Suleiman, amesema Idara na Mamkala ya Mazingira ambazo zimo ndani ya Wizara yake, zitahakikisha zinakuwa karibu na Wananchi na maeneo athirika ili kuleta suluhisho la kudumu.
Akishukuru ujio wa Makamu wa Kwanza wa Rais, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud, amesema Ziara hiyo imekuwa ya kheri na faraja kubwa, kutokana na udhia wa athari za kimazingira zinazodhoofisha juhudi za maendeleo ya eneo hilo, na tishio kwa Nchi nzima.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magharib 'A', Bi. Suzane Peter Kunambi, amesema Mamlaka yake imechukua kile alichokiita 'initiatives' na juhudi za awali, kwanza kwa kuwahamisha wananchi wa maeneo hayo, waliopatwa na athari za maporomoko, kabla ya kuwaandalia utaratibu wa kudumu utakaowapatia ahuweni ya majanga, katika maisha ya baadae.
Watendaji pamoja na Viongozi mbali mbali wa Serikali na Jamii, wamejumuika katika Ziara hiyo, wakiwemo Masheha, Madiwani sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A Unguja, Bw. Sadifa Juma na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Zanzibar Bw. Joseph John Kilangi.
Ziara hii ya Mheshimiwa Othman imelenga kukagua na kuona changamoto za ardhi zilizopo ambazo zinatokana na mabadiliko ya tabianchi hasa kwa mnasaba wa hatua mbali mbali za kibinaadamu, ndani ya Visiwa vya Unguja na Pemba.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Septemba 06, 2023.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.