RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar bado
ina mahitaji makubwa ya uwekezaji kwenye sekta ya Uchumi wa Buluu kupitia
Utalii, Uvuvi na ufugaji wa vifaranga vya samaki, Bandari, Mafuta na gesi
pamoja na sekta ya usafirishaji wa majini.
Dk. Mwinyi aliyasema
hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na mabalozi wateule waliofika
kujitambulisha, kupokea nasaha pamoja na kuaga kuelekea vituo vyao vya kazi kwenda
kuiwakilisha Tanzania Kimataifa.
Rais Dk. Mwinyi aliwanasihi
mabalozi hao kuzichangamkia fursa za uwekezaji huko kwenye vituo vyao vya kazi
na kuzileta nchini ili kuiimarisha Utalii wa Zanzibar ambao nitegemeo kwa uchumi
wa nchi unaochangia asilimia 30 ya pato la taifa.
Aliwataka mabalozi
hao kuangalia zaidi soko jipya la utalii mbali na kutangaza utalii wa fukwe na
Urithi lakini pia kuangalia fursa mpya za utalii wa mikutano, michezo na
uwekezaji ili kuitangaza zaidi Zanzibar na kuiingiza watalii wengi wa maeneo
mengine ya dunia ikiwemo China ambayo ina watalii wachache Afrika.
Kuhusu sekta ya Uvuvi
na ufugaji wa Samaki Rais Dk. Mwinyi aliwataka
mabalozi hao kuitangaza zaidi fursa hiyo pamoja na kutafuta wawekezaji
na masoko ya kilimo cha Mwani ambapo Zanzibar inaongoza kwa kuzalisha mwani
Afrika pia aliwataka Mabalozi hao kuangalia fursa ya masoko ya bidhaa za
Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ikiwemo mazao ya viungo.
Pia Rais Dk. Mwinyi
aliwaelekeza Mabalozi hao kuzichangamkia fursa za fedha, mitaji na mikopo
pamoja na kuimarisha ushirikiano mwema kwa nyanja zote zikiwemo elimu ili
kubadilishana uzoefu baina ya Tanzania na mataifa wanayokwenda kuiwakisha huko
duniani.
Sambamba na hayo pia
Rais Dk. Mwinyi aliizungumzia fursa ya Bandari jumuishi kwa Zanzibar kwa sasa inahitaji
Bandari kubwa ili kukidhi mahitaji ya uchumi wake kama kituo muhimu cha
usafirishaji, usambadhi wa bidhaa kutoa huduma na kufanyia biasha ikiwemo
kupokelea mizigo, kusafirishia mazao, na mahitaji mbalimbali ikiwemo mafuta,
nafaka, na kukuza uchumi wake.
Akizungumzia suala la
mafuta na gesi pamoja na sekta ya usafirishaji wa majini, Rais Dk. Mwinyi
alieleza Zanzibar inahitaji uwekezaji mkubwa kwenye sekta hiyo ili kuimarisha
sekta ya biashara na uchumi wake kupitia bandari za Zanzibar, Pemba, Tanga, Dar
es Salaam, Mtwata, mengine wakiwemo Msumbiji, visiwa vya komoro na kwengineko.
“Zanzibar inahitaji
vyombo vya usafiri wa majini kwa safari za Pemba, Tanga, Dar es Salaam, Mtwara na
kwengineko kama Msumbiji, Komoro na sehemu nyengine za visiwa nilizonungukwa na
bahari kwa maeneo karibu, Uchumi wa Buluu umejikita kwenye maeneo mengi ya
uchumi unahitaji wawekezaji” Alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.
Hata, hivyo Rais Dk.
Mwinyi aliwataka Mabalozi hao kuendelea kuimarisha ushirikiano mzuri na
kuimarisha ujirani mwema uliopo kwa watakaoiwakilisha Tanzania kwenye nchi
jirani sambamba na kuwaahidi ushirikiano mzuri mabalozi hao baina yao na
Serikali ya SMZ ili kutekeleza vyema majukumu ya kazi zao.
Kwa upande wao
mabalozi hao walimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kuzifanyia kazi nasaha na maelekezo
aliyowapa wakati wote wa utumishi wao na kumuahidi kuchangamkia vyema fursa
zilizomo kwenye maeneo yao ya kazi kwa lengo la kuendelea kuiimarisha
Diplomasia ya Uchumi na kuiendeleza kwa vitendo Sera ya Uchumi wa Buluu.
Akizungumza kwa niaba
ya mabalozi wenziwe, Balozi Khamis Mussa Omar anaekwenda kuiwakisha Tanzania
jijini Beijing, China alimuahidi Rais Dk. Mwinyi mbali na kuzichangamkia fursa za uchumi na
uwekezaji kwenye vituo vyao vya kazi alimuhakikisha Rais Dk. Mwinyi watakwenda
kuboresha zaidi uhusiani na ushirikiano wa kidiplomasia uliopo baina ya
Tanzania na mataifa hayo pia kuimarisha ujirani mwema wa Mabalozi wa vituo
vilivyopo kwenye nchi jirani kwa kuhakikisha wanasimamia usalama wa nchi na
kukuza uchumi na biashara baina yao.
Mabalozi wengine ni
Balozi Hassan Mwamweta anaekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Ujerumani na
mataifa ya Bulgaria, Czech, Hungary, Old Swiss, Poland, Slovakia na Switzerland.
Wengine ni Balozi,
Habibu Awesu Muhamed anaekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Qatar, Balozi
Mohamed Juma Saudi Arabia, Imani Njikai Algeria, Balozi Meja Jenerali Ramson
Mwaisaka atakaeiwakilisha Tanzania nchini Misri, Balozi Gelasuis Byakanwa
ataiwakilisha Tanzania nchini Burundi na Balozi Dk. Benard Kibesse
ataiwakilisha Tanzania jijini Nairobi, Kenya
Mabalozi hao nane waliapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan Agosti 16 mwaka huu baada ya kuwateua kushika nafasi hizo Mwezi Mei mwaka huu.
No comments:
Post a Comment