Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk Hussein Mwinyi akutana na kuzungumza na Balozi wa Finland Nchini Tanzania

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza mgeni wake Balozi wa Finland Nchini Tanzania Mhe.Theresa Ztting, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 11-10-2023.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika akizungumza na mgeni wake Balozi wa Finland Nchini Tanzania Mhe. Theresa Zitting, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika Ukumbu wa Ikulu leo 11-10-2023.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na mgeni wake Balozi wa Finland Nchini Tanzania Mhe. Theresa Zitting, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 11-10-2023.(Picha na Ikulu)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Serikali ya Finland kwa jitihada zake za kuiunga mkono Zanzibar na kuisaidia kwenye masuala mbalimbali ya uchumi na Maendeleo.

Dk. Mwinyi alitoa shukurani hizo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Balozi wa Finland nchini, Theresa Zitting.

Alisema hatua ya Serikali ya Finlanda kuisaidia Zanzibar kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Elimu, Kilimo, Afya, masuala ya wanawake hasa mapambano dhidi ya udhalilishaji wa jinsia kwa kushirikiana na taasisi na wanaharakati mbalimbali wanaopinga udhalilishaji wa wananwake na watoto.

Akizungumzia sekta ya utalii, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi huyo juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuiimarisha sekta hiyo inayochangia asilimia 30 ya pato la taifa.

Alisema, Zanzibar inaimarisha Sera yake kuu ya Uchumi wa Buluu inayobeba mambo matano ikiwemo Utalii, Uvuvi, Usafiri wa vyombo vya bahari, Bandari, Mafuta na gesi na kumueleza Balozi huyo kuangalia fursa za uwekezaji kwenye maeneo hayo.

Alisema sekta ya Utalii inajumuisha fukwe  nzuri nyenye mvuto wageni pamoja na utalii wa urithi na kuongeza kuwa kuna fursa nyingi za uwekezaji hivyo alimueleza Balozi hyo kuangalia namna ya kuzitumia fursa hizo.

Akizungumzia sekta ya Uvuvi, Rais Dk. Mwinyi alimweleza mgeni huyo kwamba Zanzibar imejikita zaidi kwenye kilimo cha viumbe wa baharini ikiwemo ufugaji wa samaki na vifaranga, matango ya bahari na ukulima wa mwani ambao umewamuisha sehemu kubwa ya wanawake na vijana na kupunguza changamoto za ajira.

Kuhusu Usafiri wa vyombo vya baharini Dk. Mwinyi alieleza unajumuisha bandari za Zanzibar, Dar es Salaam Pemba na Tanga kwa kusafirisha abiria na mizigo hivyo alieleza kuna fursa nyingi za uwekezaji kwenye eneo hilo.

Pia Rais Dk. Mwinyi alimueleza balozi huyo, kuangalia ushirikiano wa kuiungamkono Zanzibar kwenye miundombinu ya elimu, afya na nishati hasa kwenye masuala ya mifumo na vitendea kazi.

Naye, Balozi Theresa Zitting alimueleza Dk. Mwinyi kwamba Serikali ya Finland inafanyakazi kwa karibu zaidi na Serikali ya Zanzibar ambayo wanashikiriana kwenye Masuala mbalimbali ya maendeleo.

Alisema Finland imeshirikiana sana na Tanzania hasa kwenye sekta za Elimu,  na kuimarisha miradi mingi ikwemo uhifadhi wa mazingira, ardhi, misitu na masuala mengine ya maendeleo.

Balozi Zitting alisema Finland inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo baina yao na Tannzania ikiwemo Zanzibar pamoja na nchi zote zilizopo Afrika Mashariki.

Balozi Theresa Zitting yupo nchini tokea mwezi Septemba mwaka 2022 kwenye ubalozi wao uliopo Dar es Salaam.

IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.