Habari za Punde

Tuunge mkono kwa dhati kuanzishwa mfuko wa huduma za afya Zanzibar

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) Yassir Omar Juma akizungumza na Maafisa Tehama  na Utumishi  kuhusu kuboresha  usajili wa wanachama kupitia  mfumo wa huduma za Afya  hafla iliyofanyika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe, Hassan Khamis Hafidh akifungua mafunzo kwa Waandishi wa Habari kuhusiana na kuanzishwa kwa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar hafla iliyofanyika  katika Ukumbi wa  Michenzani Mall  
Waandishi wa Habari  kutoka Vyombo mbalimbali wakipatiwa mafunzo juu ya  kuanzishwa kwa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF)katika Ukumbi wa (ZHSF)  Michenzani Mall.

Na Rahma Khamis, Maelezo

Ule Usemi wa wahenga usemao “Unda Chako uweze kutumia hadi usahau cha wenzako” Usemi huu ulitumika sana katika kipindi cha wahenga ambao walikuwa wakiutumia katika kuthibitisha umuhimu wa kuthamini, kupenda kujitahidi kutumia chao, hadi kusahau cha wenzao .

Kufuatia usemi huo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, awamu ya nane chini ya uongozi wa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, imeamua kuanzisha rasmi taasisi ya Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF)kwa kuonyesha jinsi inavyowajali wananachi wake Unguja na Pemba.

Mfuko huo haukuanzishwa tu kibubusa bali ni kwa mujibu wa sheria ambapo sheria namba 1 ya mwaka 2023, ilielekeza  kuwapatia wazanzibar huduma bora za matibabu Nchini.

Ulimwengu wa sasa, taifa lolote linahitaji wananchi wake wawe na afya bora na za uhakika , kwa ajili ya kuzalisha na kutoa huduma bora, kwa dhumuni la kuinua uchumi wa wanajamii na  taifa kwa ujumla.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, awamu ya nane, imeanzisha mfuko huo baada ya kufanya tathimini mbalimbali na kupata mafunzo kwa baadhi ya watumishi na watendaji wa serikali katika sehemu tofauti Ulimwenguni.

Kwa kweli unda  chako utumie hadi usahau cha mwezako sasa tunaunda mfuko wetu unaofana na Mifuko katika Nchi zilianza kutoa huduma za Afya kuoitia mifuko hiyo.

mfano wa wazi ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) uliopo Tanzania Bara njia walizopitia mfuko huu ndio hizohizo zinazoenda kusimamia Mfuko wa ZHSF.

 Miongoni mwa nchi zenye mifuko hiyo ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda na Mataifa mengine mbalimbali ya Afrika Mashariki na duniani.

Lengo hasa la kuanzishwa mfuko huo muhimu hapa nchini, ni kuwarahisishia wananchi huduma bora na za uhakika, ili Zanzibar iweze kuwa na watu wenye afya njema na nzuri, watakaoweza kufanya shughuli na kazi mbalimbali za uzalishaji na utoaji huduma bora kwa jamii.

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidh, amesema lengo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar awamu ya nane ni kuhakikisha wananchi karibu wote wa Visiwa vya Unguja na Pemba, wanapata huduma za afya zilizobora na za uhakika kwa lengo la wanajamii hao kuweza kuondokana na maradhi mbalimbali kwa matarajio ya kuzalisha na kufanya nchi na wananchi wake kuwa wenye ubora.

“Mfuko wa huduma za afya Zanzibar, utasaidia kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi wenye kipato cha chini, cha kati na ambao hawana uwezo wa kulipia huduma za matibabu kwenye vituo vya afya, Zahanati na hospitali kutokana na hali zao, jambo ambalo Serikali ya Mapinduzi awamu ya nane chini ya Dk.Rais  Hussein Mwinyi imeweza kulipatia ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo” Naibu Waziri alifahamisha.

Naibu alifafanua kuwa kwa mujibu wa utafiti wa kisayansi uliyofanyika katika mataifa mbalimbali yenye mifuko hiyo, imeonesha kwamba wanajamii wa nchi hizo,kwa asilimia 25.6 ya watu wote waliyofanyiwa tafiti hiyo hawana uwezo wa kulipia matibabu.

“ Kabla ya kufanya maamuzi ya kuanzisha mfuko wa huduma za afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imejiridhisha vya kutosha juu ya watu wake kuweza kumudu gharama za matibabu kwa kuangalia kipato cha wananchi wa Zanzibar”, alisisitiza Naibu Waziri Hassan Hafidh.

Naibu Waziri, alikumbusha kwamba kwa kuthamini na kuwapenda wananchi Serikali ya Mapinduzi, awamu ya nane chini ya jemadari mahiri Dk, Hussein Mwinyi, imeamua kubuni mfuko wa huduma za afya Zanzibar (ZHSF), kwa lengo la kuwapatia unafuu wananchi, na kuhakikisha wanatoa  huduma bora na za uhakika kwa Wananchi.

Alifahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, itaweza kuwasaidia wale ambao hawatakuwa na uwezo wa kuchangia mfuko huo.

“ Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itawajibika kuwachangia watu wake katika mfuko wa huduma za afya, kwa ajili ya kuimarisha afya wananchi wa Visiwa vya Unguja Pemba” alifahamisha Naibu wa Waziri wa afya.

Alijulisha kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, tayari imeshajipanga kikamilifu katika kuhakikisha wananchi wote wa Zanzibar wanafaidika na huduma kupitia mfuko huo.

Aliongeza kwamba kuna kila sababu ya wananchi kuupokea ipasavyo mfuko wa huduma za afya, kwani utaweza kupunguza gharama za matibabu kwa watu wenye kipato cha chini.

“Katika kuthibitisha hayo ndiyo maana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejenga hospitali, vituo vya afya na Zahanati kadhaa kwenye nchi yetu, kwa wakaazi wa mjini na Mashamba, ili kupunguza ugonjwa na maradhi mbalimbali” aliongeza Naibu Waziri.

Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko huo Yassir Ameir Juma, amesema kuwa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar ni mwarobaini kwa wananchi kuweza kumudu gharama za matibabu nchini.

“Kuwa kuanzishwa kwa Mfuko huo kutawasaidia wananchi wote wa Zanzibar kupata huduma bora na za uhakika bila ya kubagua na kuwatoa hofu baadhi watu wenye wasiwasi na mfuko katika kutoa huduma hizo” alijulisha Kaimu  Mkurugenzi.

 na kuwataka wananch hao kujunga na Mfuko huo.

Amefahamisha kwamba mfuko wa huduma za afya Zanzibar hautaweza kuishi katika Visiwa vya Unguja na Pemba tu, bali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa dhamira ya kutoa huduma bora na za uhakika kwa wote wenye sifa.

“Huduma zote za msingi zitakuwepo katika mfuko huo, ili kuepusha usumbufu kwa wagonjwa ambao wanahitaji matibabu” alifahamisha Kaimu huyo.

Alisisitiza kwamba endapo mwananchi mwenye ugonjwa lazima anapaswa kupata huduma hizo kituo cha karibu na siyo jambo jemba kwenda hospitali za ngazi za juu, kabla ya kupitia kuanzia chini. 

“Endapo hatutaweka utaratibu mzuri na wakueleweka gharama kubwa zitaweza kutumika na ili mfuko huo uendelee kufanyakazi kwa ufanisi ni lazima utaratibu huo utumiwe kikamilifu, kwani mfuko huo unahitaji kulindwa kwa dhamira ya kuanzishwa kwake” alikumbusha, Kaimu Mkurugenzi,  Yassir.

Alitoa wito katika vituo vya afya na hospitali kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa, kwa ajili ya kuepusha malalamiko kutoka kwa wapata huduma ambao wanamatarajio makubwa na mazuri kwa mfuko huo.

“ Wito wangu kwa watoa huduma za afya wawe na lugha nzuri kwa wagonjwa wanaofika kwenye sehemu zao, ili kuepusha malalamiko na manung’uniko yasiyo kuwa na ulazima” alisisitiza.

Amesema kuwa mfuko huo utaweza kutumika kwa Tanzania Bara na Zanzibar, kwani Serikali ya Mapinduzi imeshafanya mazungumzo na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo mazungumnzo hayo yanaendelea vizuri, hivyo kuwatoa hofu wananchi wanaotumia mfumo wa Bima ya Afya ya huko.

“ Nawatoa hofu na wasiwasi wananchi wote wanaotumia mfuko wa Bima ya Afya ya Tanzania, kwamba tumefanya kila juhudi kuhakikisha wajamii wa taifa hawaathiriki kuanzisha kwa mfuko wa afya Zanzibar, wataweza kujipatia huduma popote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” amefahamisha Kaimu huyo.

Hivyo ndugu wananchi nawashauri ni jambo la busara kwa watu wote Zanzibar kujiunga na mfuko huo, ili kuishi kwa kujiamini hata pale unapopata dharura ya kupata ugonjwa ama maradhi makubwa ya kiafya, utaweza kutibiwa kwa mfuko. Shime Wananchi tuunge mkono kwa dhati mfuko wa huduma za afya Zanzibar, kwani ni mkombozi mkubwa wa maisha yetu. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.