Habari za Punde

Tuziishi alama za Mtume Muhammad ili kupata mafanikio - Mhe Othman

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, akisalimiana na Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj  Walid Alhad Omar Kawambwa; wakati alipohudhuria Maulid Matukufu ya Kuadhimisha Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W.), huko Viwanja vya Al Abbassiya, Mtaa wa Mkunguni na Likoma, Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Jijini Dar es Salaam, Tanzania Usiku wa jana Oktoba 12, 2023 

 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, akisalimiana na Mufti Mkuu wa Tanzania, Alhaj Sheikh Abubakar bin Zubeir bin Aliy; wakati alipohudhuria Maulid Matukufu ya Kuadhimisha Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W.), huko Viwanja vya Al Abbassiya, Mtaa wa Mkunguni na Likoma, Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Jijini Dar es Salaam, Tanzania Usiku wa jana Oktoba 12, 2023.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, akiwa pamojaViongozi wa Dini ya Kiisalamu wakati alipohudhuria Maulid Matukufu ya Kuadhimisha Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W.), huko Viwanja vya Al Abbassiya, Mtaa wa Mkunguni na Likoma, Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Jijini Dar es Salaam, Tanzania Usiku wa jana Oktoba 12, 2023, kushoto kwa Mheshimiwa Othman ni Mufti Mkuu wa Tanzania, Alhaj Sheikh Abubakar bin Zubeir bin Aliy na kulia kwake ni Kiongozi wa Kituo cha Kiislamu cha 'Al-Abbassiya Islamic Centre (AIC) cha Jijini Dar es Salaam, Sheikh Abbass bin Ramadhan bin Abbass.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, akitoa Salamu zake kwa Viongozi, Wananchi na Waumini wa Kiislamu wakati alipohudhuria Maulid Matukufu ya Kuadhimisha Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W.), huko Viwanja vya Al Abbassiya, Mtaa wa Mkunguni na Likoma, Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Jijini Dar es Salaam, Tanzania, Usiku wa jana Oktoba 12, 2023 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Alhaj Othman Masoud Othman, amesema Ulimwengu unahitaji kuziishi Alama za Uislamu ambazo aliziwacha Mtume Muhammad (S.A.W.) ili Dunia ibaki kuwa na mafanikio na pahala bora pa kuishi.

 

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo Usiku wa Kuamkia Leo akitoa Salamu zake kwa Viongozi, Wananchi na Waumini wa Kiislamu wakati alipohudhuria Maulid Matukufu ya Kuadhimisha Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W.), huko Viwanja vya Al Abbassiya, Mtaa wa Mkunguni na Likoma, Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Jijini Dar es Salaam, Tanzania.

 

Mheshimiwa Othman ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wa Hafla hiyo amesema  Alama hizo ni Utajiri Mkubwa kwa Umma wa Kiislamu pamoja na Ulimwengu wote, licha ya kwamba Waislamu wenyewe wamezikiuka na hivyo kupoteza murua hali ambayo imepelekea kudhoofika kwa jamii na  Umma wote.

 

 

Akitolea mfano utajiri katika Mwenendo wa Kiislamu, ambao umeleta mazingatio na manufaa makubwa kwa ulimwengu na watu, hata wasiokuwa wafuasi wa Dini hii, Mheshimiwa Othman amemtaja Mwandishi Mashuhuri wa Vitabu Duniani, Robin Sharma, ambaye ameweza kupata maslahi makubwa kutokana na Uandishi wake kuhusu 'Faida za Funga kwa Afya ya Mwanadamu'.

 

 

Katika Salamu zake hizo Mheshimiwa Othman  amesema Alama za Mtume (.S.A.W.) zikiwemo Mafunzo  , Miongozo bora na Tabia Njema, zimekuwa kimbilio hata kwa Wasiokuwa- Waislamu ambao wamejaribu kuzifuatilia na kujiwekea dira zao za Maisha, ikiwemo Mifumo ya Taaluma, Utawala na Maendeleo yao ya Kiuchumi hata katika zama za sasa.

 

 

"Dini yetu ina Alama nyingi sana zenye utajiri na hazima kwa ulimwengu wote, lakini Alama kubwa zadi ni Mwenendo wa Mtume wetu Muhammad Swallallahu Alayhi Wassallam", amesema Mheshimiwa Othman.

 

 

Hivyo amesema ni wajibu kwa Waumini wa Kiislamu kuzingatia na kumuweka Mtume (S.A.W.) nyoyoni  pamoja na kuyaendeleza kwa vitendo na katika Ngazi zote za Jamii, Mafunzo aliyokuja nayo Mtume (S.A.W.) kwani yeye alikuwa ni Qur-an inayotembea kutokana na mwenendo wa akhlaq zake njema.

 

 

"Lakustaajabisha na la kusikitisha ni kwamba yale mambo ambayo ni Alama muhimu za Uislamu kupitia kwa Mtume Muhammad (S.A.W.) Waislamu wamezikiuka na hivyo kupoteza mwelekeo, kwani ukishindwa kufutata Mwongozo uliosahihi, basi utawekewa mambo ya kufuata yasiyokuwa sahihi", amefahamisha Mheshimiwa Othman.

 

 

Ametaja mambo ambayo yameporomosha murua wa Waislamu kwamba ni pamoja na ubadhirifu, matumizi mabaya ya teknolojia, kuporomoka kwa maadili ya Vijana na pia kuporomoka kwa 'ihtiraam' heshima ya mwanamke katika jamii na dunia ya sasa kwa ujumla.

 

 

Akibainisha kwamba mambo hayo ni katika yale yaliyopelekea kuanguka kwa Dola ya Kiislamu iliyokuwa chini ya Ufalme wa Ottoman Nchini Uturuki, Mheshimiwa Othman amehimiza kwa kusema, "iwapo haya hatutoyarithisha na kuyakaririsha kwa watoto wetu itakuwa ni vigumu kwa jamii ya kiislamu kukabiliana na mabadiliko ya sasa na ya baadae ulimwenguni na kwamba huko tunakokwenda ni kugumu".

 

 

Hata hivyo Mheshimiwa, ametoa shukrani zake za dhati kwa Waandalizi wa Hafla hiyo na Mshabaha wake akisema hizo zinatoa mchango mkubwa kwa jamii katika kutukuza, kutangaza na kurithisha Alama za Uislamu.

 

Naye, Mufti Mkuu wa Tanzania, Alhaj Sheikh Abubakar bin Zubeir bin Aliy amewahimiza Waislamu kuzidisha Mapenzi kwa Kiongozi wa Umati huu, Mtume Muhammad (S.A.W.) ili kupata mafanikio zaidi.

 

 

Katika Risala yao, Waandalizi wa Maulid hayo, wamewashukru Waumini kwa Misaada mbalimbali, huku wakiuhamasisha Umma wa Kiislamu, kuelekeza nguvu zao katika kuungamkono azma na harakati  za Kituo hicho, zikiwemo za kuwaendeleza vijana kitaaluma, Maadili, Elimu ya Dini ya Kiislamu na katika nyanja zote muhimu za maisha.

 

 

Waislamu kutoka Dar es Salaam na Mikoa ya Jirani,  Viongozi mbalimbali wa Serikali, Jamii, Dini, Vyama vya Siasa,  Wakuu wa Taasisi za Kiislamu wakiwemo waliotoka Nchini Kenya, Wanamadrasa na Walimu, Masheikh na Ulamaa mbalimbali wakiongozwa na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar, Sheikh Abdulla Talib Abdulla;  Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj  Walid Alhad Omar Kawambwa; na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, wamehudhuria katika hafla hiyo.

 

 

Maulid hayo yaliyoambatana na harakati mbalimbali zikiwemo za Mawaidha, Anasheed, Milango ya Barzanj, Matayassar ya Qur-an Tukufu, Visomo  pamoja na Dua Maalum, na ambayo hufanyika kila Mwaka,  yameandaliwa na Kituo cha Kiislamu cha 'Al-Abbassiya Islamic Centre (AIC) cha Jijini Dar es Salaam, chini ya Kiongozi wake Mkuu, Sheikh Abbass bin Ramadhan bin Abbass.

 

 

 

Kitengo cha Habari,

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,

Ijumaa, Oktoba 13, 2023.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.