Na. Mwandishi na OMKR.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kwamba Zanzibar inazo rasilimali za kutosha kuweza kuzalisha fedha nyingi, lakini zinahitaji kuingizwa kwenye Mfumo rasmi wa kiuchumi utakaosaidia ukuzaji uchumi ili kuleta maendeleo ya haraka.
Mhe. Othman ameyasema hayo ofisini
kwake Migombani mjini Zanzibar alipozungunza na Uongozi wa Taasisi ya Wahasibu,
Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi Zanzibar waliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi
hiyo ndugu Juma Amour Mohammed walofika ofisini kwa Makamu kujitambulisha baada
ya taasisi hiyo kundwa hivi karibuni.
Mhe. Makamu amesema kwamba kuwepo
kwa chombo hicho ni muhimu katika kusimamia maendeleo ya ukuzaji uchumi wa
kileo hapa Zanzibar na duniani kwa jumla, lakini lazima rasilimali za kifedha
zilizopo kuingizwa katika mfumo nzuri na
sahihi ili kuongeza uwezo wa rasilimali fedha zinaopatikana katika biashara na uwekezaji wa aina mbali mbali.
Amefahamisha kwamba nchi nyingi
duniani zimeweza kupiga hatua kubwa ya kiuchumi na kimaendeleo kutokana na
kuwepo mifumo na taratibu bora inayowezesha fedha kupatikana kwa wingi kwa vile
wawekezaji watajenga imani sahihi na mifumo iliyopo nchini.
Aidha amesema kwamba chombo hicho
pia ni muhimu katika kusaidia kuwawezesha wataalamu wa ndani wa kada za fedha,
biashara na ukaguzi wanaoweza kusimamia vyema taaluma yao kiushindani katika
ngazi za kitaifa na kimataifa na hivyo nchini kunufaika katika suala zima la
ajira kwa ndani na nje ya nchi.
Mhe. Othman ametahadharisha Taasisi
hiyo kwamba kunahaja ya kuwajengea uwezo wanaaluma wao, sio tu kwa kuzingatia viwango vya elimu ya
darsani, lakini pia kuthamini wenye ujuzi na maarifa mapana ya kuweza kutambua
na kumudu vyema majukumu yao kupitia mawanda mapana waliyonayo katika kuifahamu
mifumo na taratibu za dunia za kiuchumi unaolenga ushindani kwenye shughuli za
kibiashara na uzalishaji ndani nanje ya nchi.
Akizungunzia
suala la taaluma ya Kodi ,Mhe. Othman ameutaka uongozi wa Taasisi hiyo
kuhakikisha kwamba wanawajenga wanataaluma hiyo katika misingi mipya ya
kodi itakayowezesha kusaidia kuchangia
ukuaji wa uchumi wa Zanzibar kwa haraka kama zilivyoweza kufanikiwa nchi
nyengine mbali mbali duniani.
Naye
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi hiyo ya Wahasibu, Wakaguzi na
Washauri Elekezi wa Kodi Zanzibar ndugu Juma Amour Mohammed kwamba Taasisi hiyo
inalenga kuijenga kada hiyo katika kufuata na kuzingatia maadili ya kifedha
ambayo yameonekana kupotea.
Aidha
amesema kwamba watendaji wengi walikosa kujiamini na kutokuwepo uadilifu katika
utendaji wa majukumu yao ikiwemo uandishi wa ripoti za kifedha na kwamba kuwepo
kwa taasisi hiyo kutawezesha kusimamia vyema maadili na taaluma ya kiuhasibu Zanzibar.
Amefahamisha
kwamba kadri siku siku zinavyokwenda mbele
kunaendelea kutokea mabadiliko makubwa katika kada ya fedha na biashara
na ndio maana tayari hapa Zanzibar kumeanzishwa
benki za kiislamu na bima zinazozingatia misingi ya kislamu mambo ambayo
yanahitaji kujengewa uwezo ili shunguli za kitaaluma ziweze kufanyika vyema na
kufikia lengo la ufanisi.
Naye
Mkurugenzi wa Taasisi hiyo ndugu Ame
Burhan Shadhili amesema kwamba ofisi hiyo inakusudia kuongeza ubora wa huduma
zinazotolewa na wanachama wa taasisi kwa kuwa awali hakukua na chombo kama hiyo
lakini huduma za namna hiyo zilitumiwa kutoka tanzania bara.
Wakati huo huo Mhe. Othman
amekabidhi fedha Taslim shilingi milioni mbili na laki tano kwa Waziri wa
Habari, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita ikiwa ni utekezaji wa
ahadi yake ya kuwazawadia Timu ya vijana ya Umri wa Chini ya miaka 15 kufuatia
ushindi wao wa hivi karibuni walipoifunga timu ya Uganda mabao Manne kwa matatu
kwa mikwaju ya penaliti katika mashindano ya CECAFA baada ya mchezo huo awali
kutoka suluhu ya bao moja kwa moja na Zanzibar kuibuka washindi kwa penalty.
Akipokea fedha hizo waziri wa
Habari Utamaduni na Michezo Taiba Maulid Mwita amesema kwamba mafanikio
yaliyopatikana kwa timu hiyo yametokana na mashirikiano ya viongozi na wananchi
mbali mbali jambo ambalo limeleta faraja sana kwa vijana.
No comments:
Post a Comment