Na Takdir Ali na Sabiha Khamis. Maelezo. 26.02.2024.
Kamati ya Kanuni na Sheria ndogo ndogo ya Baraza la Wawakilishi imebaini kasoro na kupendekeza kufanyiwa marekebisho na kuchukuliwa hatua.
Akiwasilisha ripoti ya mwaka 2023/2024 katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mihayo Juma N’hunga amesema kamati baada ya kupitia Kanuni hizo ilibaini kasoro mbalimbali ambazo ni kinyume na Sheria.
Amesema Baadhi ya Kanuni zilizowasilishwa katika Kamati hazikuwa zimetangazwa katika Gazeti Rasmi la Serikali jambo ambalo ni kinyume na utaratibu wa uandishi wa Kanuni hizo.
Aidha ametaja baadhi ya kasoro hizo kuwa ni pamoja na baadhi ya Kanuni zimeonesha makosa bila ya kuonesha adhabu inayotokana na kosa hilo, baadhi ya Kanuni zimeandikwa bila ya kuzingatia vifungu wezeshi vya Sheria husika na Baadhi ya Kanuni hazikuonesha uhalisia wa utekelezaji wa amri inayotolewa na Kanuni hiyo.
Hata hivyo amesema licha ya kupatikana mafanikio mbalimbali katika kutekeleza wa kazi lakini kumebainika changamoto mbalimbali ikiwemo uwasilishwaji wa baadhi ya Kanuni kwa Lugha ya Kiengereza.
‘‘Kanuni ya 25 ya Kanuni za Kudumu za Baraza la Wawakilishi, 2020, nazo zinasisitiza kuwa lugha ya Kiswahili ndio lugha rasmi ya Baraza.’’alisema Mwenyekiti huyo.
Akichangia ripoti hiyo Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia kundi la Vijana Mhe. Khudhaima Mbarak Tahir ameziomba Taasisi husika kuyafanyia kazi mapungufu yaliyobainika ikiwemo Maafisa Sheria kutofata taratibu za kanuni kwa kutowashirikisha Wadau hasa kwa upande wa Pemba.
‘‘Wadau ni walengwa wakubwa wa kuzitumia kanuni hizo hivyo natoa wito wa kufatwa na kutekelezwa kwa kanuni hizo.’’alisema Mjumbe huyo.
Kamati ya Kanuni na Sheria ndogo ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar inatekeleza majukumu yake kwa Mamlaka iliyokasimiwa na Baraza ambalo ndio chombo cha Kutunga Sheria kwa mujibu wa Ibara ya 78 ya Katiba ya Zanzibar, 1984 ambapo zinajumuisha Amri, Matamko, Kanuni za Taasisi, Kanuni za Mahakama, Kanuni za Wizara, Tangazo na Taarifa.
No comments:
Post a Comment