Habari za Punde

MBUYU EDWARD LOWASSA AFARIKI DUNIA LEO , NJIA ZAKE KATIKA SIASA NA UONGOZI HIZI HAPA..

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

MZEE Lowassa HATUNAYE,  Ndivyo tunavyoweza kuelezea taarifa za kufariki dunia kwa Mwanasiasa mkongwe na Waziri Mkuu Mstaafu  Edward Lowassa.

Taarifa za kifo cha mzee Lowassa zimetangazwa leo Februari 10, 2024 na Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango ambapo amesema amefariki akiwa katika Taasisi ya Moyo ya  Jakaya Kikwete (JKCI) ya jijini Dar es Salaam.

Dk.Mpango wakati anatangaza kifo hicho amesema "Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Edward Lowassa (70) amefariki Dunia leo February 10,2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es Salaam."

Hata hivyo kwa kukumbusha tu Waziri Mkuu mstaafu Lowassa kwa muda mrefu alikuwa kimya kutokana na kusumbuliwa na changamoto za kiafya.

Kuhusu Lowassa na Uwaziri Mkuu , ni kwamba enzi za uhai wake alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa 10 wa  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Desemba 30,  2005 na akajiuzulu Februari  7 ,  2008.

Sababu za Lowassa kujiuzulu zilitokana na kuibuka kwa kashfa ya sakata la  Richmond ambapo aliamua kuachia nafasi hiyo baada ya kuibuka kwa mjadala mkubwa ndani na nje ya Bunge, hivyo na kupelekea kuundwa kamati ya kuchunguza sakata hilo.a

Alipoona mambo yamekuwa mengi alitangaza mbele ya Bunge kwamba anajiuzulu nafasi hiyo na kwamba amebaini tatizo ni Uwaziri Mkuu.

Wakati wa sakata la Richmond Bunge liliamua kuunda Kamati ya kuchunguza sakata hilo na Dk.Harson Mwakyembe aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kyela mkoani Mbeya alikuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo na wakati huo Spika wa Bunge alikuwa Samweli Sita( sasa marehemu).

Pamoja na kujiuzulu nafasi Lowassa aliyekuwa amefanikiwa na kundi kubwa la wafuasi waliomuamini na kumpigania katika kila jambo aliendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Hata hivyo Lowassa wakati nchi inaelekea katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 aliamua  mgombea urais kupitia ndani ya Chama chake cha CCM lakini katika mchakato wa ndani ya Chama hakufanikiwa baada ya jina lake kuondolewa.

Katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 CCM ilimsimamisha Dk.John Pombe  Magufuli kugombea urais na  Lowassa baada ya kukatwa kwa jina lake aliondoka kwenye Chama hicho na kujiunga na CHADEMA ambapo alipata nafasi ya kuteuliwa kugombea Urais kupitia CHADEMA.

Wakati wa uchaguzi huo wa urais mwaka 2015 Lowassa alikuwa na ushawishi mkubwa na hivyo kuleta upinzani mkubwa dhidi ya mgombea urais wa CCM.

Kuhusu maisha ya Lowassa ni kwamba ni mwenyeji Monduli alizaliwa  Agosti 26, 1953 na baadae alifanikiwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo na aliingia bungeni kwaa mara ya kwanza mwaka 1990.

Lowassa alisoma shahada ya kwanza katika tamthilia kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, halafu shahada ya pili katika sayansi ya maendeleo ya jamii Chuo Kikuu cha Hull nchini Uingereza.

Katika enzi za uhai wake Lowassa amepata nafasi ya kushika nafasi mbalimbali zikiwemo ikiwemo ya Waziri mdogo wa mazingira na mapambano dhidi ya umaskini katika ofisi ya Makamu wa Rais (1988-2000).

Pia Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (1989-1990), Waziri mdogo wa haki na mambo ya Bunge katika ofisi ya Makamu wa Rais (1990-1993), Mbunge wa Monduli tangu mwaka 1990 na Desemba 2005 alipitishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na ilipofika mwaka 2015 aligombea  Urais.

Katika harakati za kisiasa mwaka  2014 Lowassa alisimamishwa na kamati kuu ya CCM baada ya kushtakiwa ya kwamba aliwahi kuanzisha kampeni ya kuwa mgombea wa urais kabla ya kipindi kilichokubaliwa na chama hiki.

Mei 2015 hatimaye aliweza kuanzisha kampeni yake rasmi lakini kamati kuu ya CCM ilimwondoa katika orodha ya majina yaliyopelekwa kwa uteuzi huu ndani ya chama.

Lowassa akaondoka katika CCM na Julai 28 Julai 2015 alijunga rasmi na chama cha upinzani cha CHADEMA.Siku chache baadaye aliteuliwa kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CHADEMA mnamo Oktoba 2015.

Kadiri ya Tume ya Uchaguzi alishindwa kwa kupata asilimia 39.97 za kura zote na mgombea wa CCM John Pombe Magufuli aliyepata asilimia 58.46.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.