Habari za Punde

Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi inaendelea kuweka mazingira rafiki

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,amesema Serikali ya awamu ya nane chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi inaendelea kuweka mazingira rafiki ya kuimarisha sera na sheria zitakazowawesesha wafanyabiashara nchini kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Hayo ameyasema wakati akizungumza katika mwendelezo wa mahojiano ya kipindi maalum kinachorushwa na Radio Bahari FM huko Migombani Zanzibar.

Amesema Rais Dk.Hussein Mwinyi,amedhamiria kufanya Mapinduzi makubwa katika sekta ya biashara nchini ili kuwapa uhuru mpana wafanyabisha kutoa huduma bora kwa Wananchi pamoja na kulipa kodi kwa wakati.

Mbeto,alisema kupitia Mkutano Mkuu 15 wa Wafanyabiashara Zanzibar(ZNCC) ,  Rais Dk.Mwinyi alifafanua kuwa wajibu wa Serikali ni kuweka mazingira bora ya kufanya biashara na kusisitiza kuwa haki ya wafanyabiashara hao ni kulipa Kodi ili isaidie katika uendeshaji huduma za kijamii.

"Serikali inategemea kodi katika kujenga Hospitali,miundombinu ya maji safi na salama,skuli,umeme na huduma zingine za kijamii yote hayo yanahitaji fedha ni lazima wafanyabiashara wawe wazalendo na wakweli katika kutekeleza wajibu wao kisheria.

Pia nawashauri Jumuiya ya wafanyabishara Zanzibar (ZNCC) wasiangalie wafanyabiashara wakubwa tu pia waangalie hata wafanyabiashara wa kati na wadogo wadogo wote wakiungana watakuwa na nguvu na maamuzi ya pamoja kuimarisha Jumuiya yao. ",alishauri Mbeto.

Katibu huyo wa Kamati Maalum ya NEC,alisema Wafanyabiashara ni chombo muhimu katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar hivyo wanatakiwa kuwa wazalendo.

Alibainisha kuwa Serikali inategemea zaidi sekta ya biashara na utoaji wa huduma kwa jamii ili zisaidie kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kukuza uchumi wa nchi.

Alieleza kuwa Kuna baadhi ya wafanyabiashara wanajali maslahi yao kwa kupandisha bei za bidhaa mbalimbali pamoja na kukwepa Kodi tabia inayoathiri mipango ya maendeleo ya nchi.

Alisema Dk.Mwinyi,amekuwa mstari wa mbele kufanya maridhiano ya kisiasa kwa dhamira ya kudumisha amani na utulivu nchini ikiwa ni sehemu ya kuweka nchi katika mazingira salama yatakayotoa fursa kwa kila mwananchi kufanya kazi zikiwemo biashara  kwa uhuru kwa lengo la kupata kipato halali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.