Habari za Punde

BAKIZA Yakutana na Wawakilishi wa Chuo cha Utamaduni Kutoka Urusi Kuimarisha Mashirikiano ya Kiswahili

Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) Dk.Mwanahija Ali Juma  akimkabidhi kitabu cha kamusi sahihi la Kiswahili na utamaduni wa mzanzibar Mwakilishi kutoka  chuo cha  utamaduni wa Urusi Maria Pateeva wakati alipotembelea Ofisi za BAKIZA kuimarisha mashirikiano, huko Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharibi B Unguja.
Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) Dk.Mwanahija Ali Juma  akipokea vitabu vya Kiswahili vilivyochapishwa nchini Urusi kutoka kwa Mwakilishi wa  chuo cha  utamaduni wa Urusi Maria Pateeva wakati alipotembelea Ofisi za BAKIZA kuimarisha mashirikiano, huko Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharibi B Unguja.
Mwakilishi kutoka chuo cha  utamaduni wa Urusi Rifat K. Pateev akizungumza na Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili Zanzibar DK. Mwanahija Ali Juma  wakati alipotembelea Ofisi za BAKIZA kwa lengo la kuimarisha  mashirikiano.


Na Rahma Khamis Maelezo
   Zanzibar. 17/4/2024

Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA)limepokea vitabu vya Kiswahili vilivochapishwa na Chuo cha Utamaduni  kutoka Urusi ili kuikuza na kuiendeleza lugha hiyo.

 

Akipokea vitabu hivyo Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dkt Mwanahija Ali Juma  amesema vitabu hivyo vitasaidia kuimarisha lugha hiyo sambamba na kujenga ushirikiano kati ya Chuo cha Utamaduni cha Urusi na Zanzibar.

  

Aidha Katibu huyo ameuomba ujumbe kutoka chuo cha Utamaduni cha Urusi kuendeleza ushirikiano uliopo kati yao ili kukieneza kiswahili duniani kote.

 

“Sisi kama baraza tuna jukumu la kuwaendeleza  waandishi wachanga na kufanya mashindano ya uwandishi wa tungo mbalimbali kwa waandishi wakubwa na wadogo ili tuhakikishe lugha yetu inatmika kwa usahihi na ufasaha”alisema Dkt Mwanahija.

 

Hata hivyo amefahamisha kuwa katika kuhakikisha lugha hiyo inafika mbali zaidi Baraza la kiswahili Zanzibar   limechanpisha makamusi na vitabu mbali mbali pamoja na  kufanya mashindano ya uandishi wa makala mbali mbali kwa waandishi wachanga na wanafunzi ili kuiendeleza lugha hiyo.

 

Mapema Dkt. Mwanahija alifahamisha  kuwa Baraza hilo ni Taasisi iliyoanzishwa chini ya kifungu nambari 4 kwa lengo la kusimamia Kiswahili na kuhakikisha kinaenda mbele na kutumika katika mawasiliano duniani kote.


Nae Mwakilishi wa chuo hicho Rifat K. Pateev amesema Urusi ndio nchi ya kwanza kuchapisha vitabu vya Kiswahili ikiwemo kitabu cha Shaaban Robert na Shafi Adam Shafi na hivi karibuni wameanza kuisomesha lugha hiyo maskulini.

 

Aidha amefafanua kwamba lugha hiyo inaendelea kusambazwa dunia nzima kwani  katika Chuo Kikuu cha Utamaduni  wanaisomesha na kuchapisha ili wakaazi wa huko waweze kuitumia na kuenea kwa kasi zaidi.


 Ameongeza kuwa kwa sasa wapo Zanzibar kwa ajili ya kujifunza zaidi lugha ya Kiswahili  pamoja na kujenga mahusiano na Wazanzibar  ili kuiendeleza lugha hiyo.

 

 Miongoni mwa Vitabu vilivyopkelewa na Baraza la Kiswahili kutoka chuo cha utamaduni wa urusi ni pamoja na kitabu cha  Ndege wa Moto ,Bila ya Mahari, Tembo,  Sudi ya Mwanadamu na Koti la Karani ambavyo vyote vimechapishwa kwa lugha ya Kiswahili na vinatumika nchini kwao.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.