Habari za Punde

MAKAMU WA RAIS AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI SAIDI YAKUBU


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu Ikulu Jijini Dar es salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam tarehe 15 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi mpya wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu aliyefika kumuaga Ikulu Jijini Dar es salaam.

Akizungumza na Balozi huyo, Makamu wa Rais amemtaka kusimamia sera ya diplomasia ya uchumi na kutafuta maeneo mapya ya ushirikiano kwa kuibua fursa zaidi za kiuchumi. Amesema dhamira ya Tanzania ni kuendeleza na kuimarisha ushirikiano mzuri uliyodumu kwa muda mrefu na Taifa la Comoro.

Pia Makamu wa Rais amemuagiza Balozi Yakubu kufuatilia utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya ushirikiano iliyopo katika sekta mbalimbali ili kufungua fursa za kiuchumi kwa pande zote mbili.

Halikadhalika amemsihi Balozi huyo kuwa na nyenzo muhimu za kazi zitakazomuwezesha kufahamu vema vipaumbele vya taifa kama vile Dira ya Taifa, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Ilani, Sera ya Mambo ya Nje, pamoja na takwimu sahihi na za msingi kuhusu Tanzania.

Amemtaka kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji pamoja na kuongeza zaidi thamani ya biashara baina ya mataifa haya mawili ambapo kwa sasa imefikia dola za marekani milioni 55.

Pia amesema ni muhimu ubalozi kuweza kutoa taarifa juu ya masuala ya huduma za afya zinazopatikana nchini ili kuwarahisishia wananchi wa Comoro wanapohitaji matibabu. Ameongeza kwamba ni vyema kuwaunganisha Watanzania wanaoishi nchini Comoro na kuwavutia  kuwekeza nchini.

Kwa Upande wake Balozi Yakubu amemshuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumteua kumwakilisha nchini Comoro ambapo ameahidi kuendeleza ushirikiano uliopo na kuimarisha diplomasia ya uchumi ikiwemo kuongeza biashara baina ya mataifa haya mawili.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Nchni (UNHCR) Bi. Mahoua Parum’s pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) Bi. Clara Makenya Ikulu Jijini Dar es salaam.

Mazungumzo hayo yamelenga kuongeza ushirikiano katika sekta ya mazingira hususani kuwasaidia wananchi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

15 Mei 2024

Dar es salaam.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.