Habari za Punde

MAKAMU WA RAIS AZINDUA KAMPENI YA MTU NI AFYA AWAMU YA PILI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba zawadi ya ushindi wa jumla uliopata Mkoa wa Iringa katika kampeni ya usafi wa mazingira Kitaifa wakati wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Kampeni ya Mtu ni Afya na Uzinduzi  Awamu ya Pili ya Kampeni ya Mtu ni Afya yaliyofanyika Kibaha Mkoani Pwani tarehe 09 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Kampeni ya Mtu ni Afya na Uzinduzi  Awamu ya Pili ya Kampeni ya Mtu ni Afya  yaliyofanyika Kibaha Mkoani Pwani.
 

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,

Leo tumekusanyika hapa Kibaha, ili kushiriki katika maadhimisho ya miaka 50 ya kampeni ya kitaifa ya MTU NI AFYA, na uzinduzi wa awamu ya pili ya kampeni hii. Katika kipindi cha miaka 50 ya utekelezaji, Kampeni hii imetoa mchango mkubwa sana katika kujenga na kuimarisha afya ya jamii.  Nakushukuru kwa dhati Mhe. Waziri ya Afya kwa kunialika kushiriki nanyi katika maadhimisho haya. Aidha, nawashukuru pia Wadau wetu wa Maendeleo ambao tumekuwa tukishirikiana na ambao wameahidi kutushika mkono katika utekelezaji wa awamu ya pili ya kampeni hii. Vilevile, nawapongeza wahusika wote kwa maandalizi mazuri. Nawashukuru pia kwa dhati wananchi wote kwa ushiriki mzuri katika maadhimisho haya. 

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,

Kwa muda mrefu, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali zinazolenga kuboresha huduma za afya nchini, kwa kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza. Kihistoria, Serikali imeendesha kampeni kadhaa zilizolenga kujenga jamii yenye afya. Mathalan, mara baada ya uhuru Serikali iliamua kupambana na maadui watatu yaani Ujinga, Umaskini na Maradhi. Katika kupambana na maadui hawa, mwaka 1973 Serikali ilizindua rasmi kampeni ya MTU NI AFYA, iliyolenga kupambana na adui Maradhi. Kampeni hii ilitekelezwa kwa hatua na kwa namna mbalimbali kwa kipindi cha takriban miaka hamsini hadi sasa.            

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,  

Katika awamu ya kwanza, kampeni ya MTU NI AFYA ilitoa msisitizo kwa magonjwa ya mlipuko hususan yale yanayotokana na uchafu wa mazingira ikiwemo kuhara, kipindupindu, homa ya matumbo, kichocho, magonjwa yanayoambukizwa kupitia njia ya mkojo (UTI) na minyoo (salmonella). Hamasa kubwa ilitolewa kwa wananchi ili wazingatie kanuni za afya bora na kuchukua hatua madhubuti za kujikinga na maradhi hayo. Njia mbalimbali, zikiwemo nyimbo, mashairi, ngoma na vyombo vya habari zilitumika kuhamasisha masuala ya usafi wa mazingira, chanjo pamoja na kuhimiza lishe bora. Katika kipindi cha miaka hiyo 50, kampeni nyingine ndogondogo zilitekelezwa, katika maeneo tofauti tofauti kama vile matumizi ya vyoo bora, kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni, elimu ya lishe bora, udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza na uchafuzi wa mazingira, matumizi holela ya kemikali na kadhalika. Kampeni hizo zilikuwa na kaulimbiu mbalimbali zenye kutoa hamasa kama vile  “usafi ni ustaarabu, unaanza na sisi”; “usichukulie poa, nyumba ni choo”; “imarisha usafi wa mazingira kuzuia uchafuzi wa maji chini ya ardhi”, n.k. 

Awamu hii ya kwanza ilifanikiwa kwa kiasi hususan kupunguza kasi ya kuenea kwa magonjwa yanayoenezwa kwa njia ya maji (water- borne diseases) na kujenga uelewa miongoni mwa wananchi juu ya namna ya kujikinga. 

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,

Awamu ya pili ya Kampeni ya MTU NI AFYA tunayozindua leo, kaulimbiu yake ni “ Mtu ni Afya: Afya Yangu, Wajibu Wangu”. Pamoja na kuendeleza kampeni dhidi ya magonjwa ya mlipuko na yale yanayotoka na uchafu wa mazingira, kampeni tunayozindua leo inajumuisha magonjwa yasiyoambukiza.  Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, katika miaka ya 80 ni 1% tu ya watanzania walikuwa na tatizo la kisukari na 5% walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu.  Lakini hivi sasa tatizo la kisukari linaathiri 9% ya Watanzania na tatizo la shinikizo la juu la damu nalo limeongezeka na kuathiri 25% ya watu wetu. Vilevile, magonjwa yasiyoambukiza yanachangia takriban 33% ya vifo vyote nchini.  Hivyo, kampeni hii inahimiza kila mwananchi atambue kwamba ni wajibu wake kujikinga na maradhi na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwake yeye mwenyewe na kwa Serikali.

Kampeni hii tunayoanza leo inahimiza mambo makuu tisa yafuatayo: (i) ujenzi na matumizi ya vyoo bora katika ngazi ya kaya, shule za msingi na sekondari, vituo vya afya na stendi kwenye njia kuu zote za usafiri; (ii) kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni nyakati zote muhimu ili kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza; (iii) uondoshaji salama wa majitaka katika ngazi ya kaya na maeneo ya Umma (iv) kutibu maji ya kunywa kwa njia ya kuchemsha au kutumia vidonge vya klorini kwa kuzingatia maelekezo ya wataalam; (v) hedhi salama kwa watoto wa kike na huduma za usafi shuleni; (vi) menejimenti ya taka ngumu katika Majiji, Manispaa na Miji midogo; (vii) elimu kuhusu mtindo wa maisha na lishe bora, ikijumuisha kufanya mazoezi ya viungo ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza; (viii) usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ikiwemo makazi ya wananchi ili kuondoa mazalia ya mbu na wadudu wanaoeneza magonjwa; na (ix) elimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi na athari zake kiafya pamoja na matumizi ya nishati safi ya kupikia.           

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,

Serikali imedhamiria kuboresha hali ya lishe na afya za Watanzania. Ibara ya 83 (o) & (w)  na 85 ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi inaitaka Serikali kuhamasisha wananchi kuhusu kinga, kudhibiti na kuzuia magonjwa mbalimbali na kuimarisha huduma za lishe kwa wanawake wajawazito, watoto na jamii na  kupunguza aina zote za utapiamlo nchini. Wizara ya Afya, tayari imeandaa Mwongozo wa Chakula na Ulaji Tanzania (2023). Mwongozo huu unafafanua kuhusu ulaji unaofaa na mtindo wa maisha unaolenga kutoa mwongozo wa chakula na lishe kwa jamii, sera za afya na kilimo, na mipango ya elimu ya lishe, pamoja na mapendekezo ya vyakula, makundi ya chakula na mipangilio ya mlo ili kuupatia mwili virutubishi muhimu kwa afya bora na kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali yenye uhusiano na ulaji.  Hali kadhalika, upatikanaji wa maji safi na salama na uwepo wa vituo vya afya vijijini kumechangia kupungua kwa matukio ya milipuko ya magonjwa hususan yale yanayosababishwa na maji yasiyo salama. 

Mabadiliko ya tabianchi, kwa upande mwingine, yana athari za moja kwa moja kwa afya na lishe ya binadamu. Katika Mkutano wa 20 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya tabianchi (UNFCCC – COP28), uliofanyika Dubai, ilielezwa bayana kuhusu mchango wa mabadiliko ya tabianchi katika ongezeko la magonjwa ya mlipuko na vifo, hususan kwenye nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara. Magonjwa kama kipindupindu, malaria na magonjwa ya mfumo wa hewa yanatarajiwa kuongezeka kutokana na ongezeko la joto, upungufu wa mvua au mvua kubwa zinazoleta mafuriko. Aidha, majanga ya mafuriko yamekuwa yakisababisha uharibifu wa miundombinu ya maji na barabara na hivyo kuleta changamoto katika usalama wa maji na hali ya chakula na hivyo kuathiri hali ya lishe. Athari hizi, zinaonesha umuhimu wa kuwekeza zaidi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kulinda afya ya jamii na uchumi wa Taifa kwa ujumla. 

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,

Ili kufanikisha awamu ya pili ya kampeni ya MTU NI AFYA na kuifanya ifikie malengo yake, napenda kutoa msisitizo wa masuala muhimu kwa makundi mbalimbali, kama ifuatavyo: 

Kwa Wizara za Afya na TAMISEMI:  Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI waziwezeshe Idara za Afya katika Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya; (i) kuimarisha mifumo na miundombinu ya kutambua, kudhibiti na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko; (ii) kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na utambuzi wa magonjwa; (iii)  kujenga uwezo wa utayari katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko (response and preparedness); (iv) kujenga uwezo wa kufanya tafiti kuhusu magonjwa mbalimbali ili kubaini jinsi yanavyosambaa, vihatarishi na tiba yake; (v) kujenga mifumo ya usimamizi na upimaji matokeo ya kampeni hii; (vi) kuimarisha utoaji wa elimu kuhusu usafi na umuhimu wa mazoezi ya viungo kupitia programu za elimu mashuleni, machapisho mbalimbali na kupitia vyombo vya habari, hususan kwa watoto na vijana ili kuwajengea tabia ya kuthamini na kufanya mazoezi wakati wote hadi watakapokuwa watu wazima. Kazi hii itahitaji uwepo wa mfumo madhubuti wa usimamizi na ufuatiliaji wa kampeni hii ili malengo tarajiwa yaweze kufikiwa. Ili kampeni hii ifanikiwe ninazitaka Halmashauri zote kuwatumia vizuri wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao pamoja na mambo mengine watawezesha kufikiwa kwa sehemu kubwa ya jamii, kuchochea mabadiliko ya tabia za wananchi na kuhakikisha usawa na urahisi katika utoaji wa huduma. 

Kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa: Mamlaka za Serikali za Mitaa ziwekeze zaidi katika kudhibiti taka ngumu hususan kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na utupaji wa taka pamoja na uondoshaji wa maji taka kwa lengo la kuimarisha usafi katika Vijiji, Miji, Manispaa na Majiji nchini. Mamlaka za Serikali za Mitaa ziongeze kasi katika ujenzi wa mitaro, uzoaji taka, kutenga maeneo mahsusi ya utupaji taka (dumping sites) na kujenga uwezo wa menejimenti ya taka. Hatua hizi ni muhimu kwa kuwa udhibiti duni wa taka ngumu na maji taka ni vichocheo vya kuenea kwa magonjwa ya mlipuko. 

Kwa Wananchi: Jukumu kubwa la wananchi ni kujikinga na magonjwa kwa kufuata maelekezo na ushauri unaotolewa na wataalam wa afya katika ngazi mbalimbali kuhusu masuala ya kiafya ikiwemo lishe bora, mazoezi ya viungo na upimaji wa afya mara kwa mara. Pili, kujenga desturi ya kufanya usafi (usafi wa mwili na usafi wa mazingira) ili kujiepusha na magonjwa yatokanayo na uchafu. Nawakumbusha wananchi wote kuwa kinga ni bora na ina gharama nafuu kuliko tiba. Ninawasisitiza pia kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii. 

Kwa Wasanii/Vikundi vya burudani:  Sanaa ina uwezo mkubwa wa kushawishi na kuwasilisha ujumbe unaohamasisha uwajibikaji. Hivyo, kwa kutumia sanaa na muziki tunaweza kuwasilisha ujumbe kwa njia ya ubunifu na yenye mvuto zaidi hasa kwa vijana. Hii inaweza kuchochea mabadiliko chanya ya tabia katika jamii yetu. Jukumu kubwa la Wasanii na vikundi vya burudani katika kampeni hii ni kutoa hamasa na kuelimisha jamii ili kuongeza uelewa na kufuata maelekezo yanayolenga kujenga afya ya jamii.  Wasanii na vikundi mbalimbali vina wajibu wa kutengeneza tungo zenye maudhui yanayobeba dhima ya kampeni hii. 

Kwa Vyombo vya habari: Katika kampeni hii, vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuhamasisha na kuelimisha jamii kwa kupeleka ujumbe kwa njia mbalimbali za kibunifu. Aidha, kampeni za vyombo vya habari zinazolenga kutoa elimu na hamasa hazina budi kuwa endelevu na zenye kupimika. Ni matarajio yangu kwamba vyombo ya habari hususan mitandao na redio za kijamii na wadau wengine vitaibeba kampeni hii ili kuwafikia wananchi moja kwa moja hadi kwenye ngazi ya kaya. Aidha, ni muhimu kuwashirikisha pia watu mashuhuri na wenye ushawishi katika jamii ili kufikisha ujumbe. 

 Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,

Baada ya kusema hayo, sasa ninayo heshima kubwa kutamka kuwa KAMPENI YA MTU NI AFYA AWAMU YA PILI yenye Kaulimbiu isemayo “Mtu ni Afya: Afya Yangu, Wajibu Wangu” imezinduliwa rasmi. 

 

Asanteni sana kwa kunisikiliza.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.