Habari za Punde

Bajaji za Umeme Vijana Mkoani Tanga Wapatiwa Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo Namna ya Matumizi Yake

Dereva wa bajaji Halfani Rashidi akiwa kwenye bajaji inayotumia umeme ambayo anafanyia shughuli zake mjini Tanga.

VIJANA wanaopatiwa mafunzo na Shirika hilo wakiwa darasani.

Ofisa Mradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Tanzania Open Innovation, Abdulwahab Issa akiongea na waandishi wa habari.

Na Hamida Kamchalla, TANGA.
VIJANA wapatao 75 walioko kwenye mifumo ya mafunzo ya ufundi stadi wamepatiwa mafunzo ya utumiaji wa tekinolojia mpya ya vyombo vya moto vya bajaji na pikipiki zinazotumia umeme jijini Tanga. 

Vijana hao ambao 40 wametokea katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) na wengine 35 kutoka SIDO pamoja na katika baadhi ya gereji jijini humo, wamepatiwa mafunzo na Shirika lisilo la Kiserikali la Tanzania Open Innovation chini ya kampuni ya ROBOTECH LABS. 

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, 0fisa Mradi wa Shirika hilo Abdulwahab Issa, amesema vijana hao wamejifunza namna ya kuona namna jinsi bajaji zinavyofungwa pindi zinapotoka viwandani lakini pia waweze kujionea mifumo ya umeme na motor vinavyofanya kazi pamoja na kutengeneza na kutumia vyombo hivyo. 

"Lengo kubwa ni vijana kuweza kupata uwezo na kujionea kwa macho namna vyombo hivi vinavyofanya kazi lakini pia watakavyokwenda kuvisimamia wakati wa kufanya kazi katika kuokoa na kujiingizia kipato katika shuhuli zao za kila siku, 

"Bajaji hii ina uwezo wa kutembea kilomita 80 hadi 100, kwa chaji iliyojaa kwa asilimia 100 kwa umeme wa sh elfu 3, hapo inaweza ikatuonesha kwamba ni namna gani unaweza kwenda ukaokoa kipato chako cha matumizi katika ununuaji wa mafuta" amesema. 

Issa amesema sambamba na hayo, wamelenga kutoa mafunzo kwa vijana hao ili kupata mafundi watakaoweza kujua kujua jinsi ya uendeshaji, uundaji pamoja na ueekebishaji wa vyombo hivyo lakini pia wasambazaji wa vyombo hivyo kama bidahaa zitakapotoka viwandani. 

"Wito wangu wa vijana wa Mkoa wa Tanga, waendelee kujitokeza pale fursa hizi zitakapotokea, hizi fursa ni adimu na ni mara chache zinapokuwa zintolewa bure kwasababu hakuna garama zozote wanazolipia, waje wajionee, wajifunze ili waje waweze kuwa mafundi, madereva ma wasambazaji wa huduma za bidhaa hizi za bajaji" ametoa wito. 

Hata hivyo amebainisha kwamba kikubwa zaidi ni katika jitihada za utynzaji wa mazingira kuhakikisha nchi inatoka kwenye matumizi ya nishati chafu na kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi hivyo kulenga kuanza kutumia tekinolojia ya nishati ya umeme na kuachana na matumizi ya mafuta. 

Baadhi ya walioshiriki mafunzo wameelezwa kwamba mafunzo hayo yamewapa mwangaza mkubwa na kuona ni jinsi gani tekinolojia hiyo inaenda kuwafanikishia katika kipato chao pindi watakapotumia bajaji hizo. 

Mwenyekiti wa waendesha bajaji Mkoa wa Tanga Rahimu Makange amesema, "kwa upande wangu nimeona hii ni fursa kubwa sana na mafunzo haya yananifanya nijione kuwa ni Injinia mkubwa sana kwa sasa, na hizi bajaji nimeona zinarahisisha mambo mengi, 

"Hazina garama kubwa, ni suala la kuhakikisha tu hukosi luku, lakini suala la kuingia sheli kupanga foleni kutafuta petroli au dizeli hakuna, na kwamba unapokuwa na umeme wa sh elfu 3 unaweza ukasafiri kutoka Tanga hadi Korogwe, lakini ni petroli matumizi yangekuwa makubwa sana". 

Naye Halfani Rashidi dereva wa bajaji jijinu Tanga amesema, bajaji hii ya umeme tayari nimeshaanza kuitumia na manufaa yake ni makubwa, kwasababu nikiwa natumia bajaji ya kawaida nilikuwa natumia zaidi ya sh elfu 15 kwa siku lakini hii natumia umeme wa sh elfu 3 kwa siku, ni rahisi sana" ameeleza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.