Habari za Punde

uchangiaji damu ni miongoni mwa mambo ya muhimu yanayotakiwa kupewa kipao mbele

Na Maulid Yussuf WMJJWW. Zanzibar.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma amesema Shughuli za uchangiaji damu ni miongoni mwa mambo ya muhimu yanayotakiwa kupewa kipao mbele kutokana na kuokoa maisha ya watu wengi ulimwenguni.

Ameyasema hayo wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku ya wachangiaji wa damu salama, yaliyofanyika katika Viwanja vya Makao Makuu ya Damu salama Sebleni Mjini Unguja, amesema hali hiyo haifungamani na mfumo wowote wa kijamii kama kisiasa, kidini, wala kikabila.

Amesema lengo la maadhimisho ya siku hiyo ni kuwashukuru, kuwapongeza, kuwajali na kuendelea kuwahamasisha wachangiaji damu na watu wengine wapya ambao wanaweza kujitolea kuchangia damu kwa hiari ili kuweza kuokoa maisha ya wengine. 

Amesema suala kuchangia damu ni jambo la kibinaadamu linalomgusa kila mtu, na ndio mana katika hafla hiyo kuna mkusanyiko wa makundi mbalimbali wakiwemo walimu na wanafunzi wa shule, vyuo, wananchi wa kawaida, viongozi wa dini, vikosi vya ulizi na usalama kama JWTZ, Umawa, Jku, Mafunzo, KVZ, KmKm, Zima tomo (KZU), Polisi pamoja na wananchi wa kawaida. 

Amesema asilimia kubwa ya watumiaji wa damu ni kina mama wajawazito hasa pale wanapopoteza damu nyingi wakati wa kujifungua, watoto chini ya umri wa miaka mitano, wahanga wa ajali na upasuaji unaohitaji kutumia tiba ya damu.

Amesema juhudi za kuelimisha jamii zaidi kuhitajika katika shuguli hizo hapa Zanzibar zinaendelea vizuri na wananchi waliowengi wanayo elimu ya wastani juu ya kuchangia damu kwa hiari, na wanajitahidi kufika katika vituo mbali mbali nchini vikiwemo Makao makuu ya damu salama hapa Amani Sebleni makabala na Nyumba za Wazee, Hospitali zote za wilaya, Mkoa na Hospitali kuu ya Rufaa Mnazi Mmoja.

Amewashukuru wale wote waliojotolea kuchangia damu kwa hiari na kuwataka kutovunjika moyo kwani hiyo ni sadaka kubwa wanayoitoa mbele ya Mola wao.

Hata hivyo amewataka kuendelea kuwahamasisha na wananchj wengine wenye uwezo wa kuchangia damu, kujitokeza kufanya hivyo ili kuokoa maisha ya watu waliokuwa hatarini kupoteza maisha.

Mhe Riziki pia ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wote kila mmoja kwa nafasi yake kuelimishana na kupiga vita vitendo vya ukatili nabudhalilishaji wa kijinsia kwani kufanya hivyo pia kutasaidia kuokoa maisha ya akina mama na watoto ambao ndio taifa la baadae.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt Habiba.... amesema zoezi la uchangiaji wa damu Zanzibar lilianza mwaka 2005 na ulianza kwa dharura, ambapo hali hiyo ilipelekea kukosa damu kwa wakati kutokana na wakati huo baadhi ya watu kuogopa kupimwa maambukizi ya ukimwi, na hivyo kupelekea kupoteza maisha kwa baadhi ya wahitaji.

Amesema hakuna tiba mbadala wa damu, ni lazima ichangiwe ili kusaidia kuokoa maisha ya wengine, hivyo amesema anawashukuru na kuwapongeza wote walijitokeza kusaidia kuchangia damu na kuwaomba kuendelea ili kukidhi uhitaji katika hospitali zote.

Akisoma risala ya wachangiaji wa damu ndugu Fatma Rashid amesema pamoja na kuashimisha siku hiyo ya wachangiaji wa damu, lakini pia ni kusherehekea kutumia kwa miaka 20 ya uchangiaji wa damu Duniani ambapo mafanikio makubwa yamepatikana katika kusaidia kuokoa maisha ya watu.

Hata hivyo amesmea kwa upande wa Zanzibar wachangiajibwa damu wamekuw wakikqbiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kutothaminika hospitali wakati wa kuhitaji kuitumia huduma hiyo kwa wagonjwa wao, kupokea kauli zisizoridhisha kwa baadhi ya wahudumu pamoja na kutoviendeleza vikundi vya wachangiaji damu na makundi malumu.

Hivyo wameomba kufanyiwa kazi kwa changamoto hizo ili kuendana na kasi ya Serikali katika kuhakikisha damu zinapafikana na kusaidia kuokoa maisha ya watu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.