Habari za Punde

TAARIFA KWA UMMA KUTOKA WEMA

Na Idara Habari Maelezo Zanzibar.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema ajira za Ualimu haziuzwi na kuwataka Wananchi kuchukuwa tahadhari ili kuepuka kutapeliwa.

 

Kwa mujibu wa taarifa iliotolewa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Khalid M. Waziri, imesema Wizara imepokea taarifa ya kuwepo watu wasiokuwa waaminifu, wanaojifanya maafisa kutoka Wizara ya elimu na kujihusisha na uwakala wa ajira kwa kuwataka Wananchi walipe fedha ili wapatiwe ajira.

 

Taarifa hiyo imesema Wizara inakanusha kuuzwa kwa ajira zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 

Hivyo imewataka Wananchi kuwa makini na kuchukuwa tahadhari kwa watu wanaojitokeza kuomba fedha kwa ajili ya kuwapatia ajira kwani taarifa zote za ajira zinatolewa na Taasisi husika.

 

Aidha taarifa hiyo imebainisha kuwa masuala yote ya ajira hupangwa na kuratibiwa na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria na Utumishi na Utawala bora.

 

Mbali na hayo, Taarifa hiyo imesema Wizara ya elimu na Mafunzo ya amali Zanzibar, inawaomba Wananchi watakaofikwa na suala hilo wasisite kutoa taarifa kwa vyombo husika ili taratibu za kisheria zichukuliwe kwa wahusika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.