Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs
Mwambegele (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 25 Julai,
2024 mkoani Geita. Kulia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Bw. Kailima
Ramadhan na kushoto ni Mjumbe wa Tume, Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu, Asina
Omar.
Na. Mwandishi Wetu, Geita.
Wananchi watakaofanya udandanyifu ili wajiandikishe zaidi
ya mara moja wanatenda kosa na wakibainika wanaweza
kufungwa jela kifungo kisichopungua miezi sita na kulipa faini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele leo tarehe
25 Julai, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari
mkoani Geita.
“Ningependa kusisitiza kuhusu suala la kujiandikisha kuwa
mpiga kura zaidi ya mara moja, jambo hili ni kosa la kisheria
kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 114(1) cha Sheria ya
Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka
2024,” amesema.
Jaji Mwambegele amefafanua kuwa kifungu hicho kinasema
mtu yeyote atakayeomba kuandikishwa zaidi ya mara moja
atakuwa ametenda kosa la kisheria na akitiwa hatiani adhabu
yake ni faini isiyopungua kiasi cha shilingi laki moja
(100,000/=) na isiyozidi shilingi laki tatu (300,000/=) au
kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na
kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja.
Katika hatua nyingine, Jaji Mwambegele amesisitiza kuwa
hakuna uwezekano wa mtu kujiandikisha mara mbili na
taarifa zake kusalia kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura kwa kuwa kabla ya kutoa nakala ya mwisho, Tume
hulisafisha Daftari kwa kuwaondoa wapiga kura
waliojiandikisha zaidi ya mara moja.
“Mara baada ya uandikishwaji wa wapiga kura kukamilishwa,
taarifa zote huingizwa kwenye mfumo wa AFIS (Automated
Finger Print Identification System) ambao huwaonesha wote
waliojiandikisha kwenye Daftari zaidi ya mara moja. Wapiga
kura wa aina hii hufutwa moja kwa moja kwenye vituo vyote
na kuwabakisha kwenye kituo alichojiandisha mara ya
mwisho,” amesema.
Ameongeza kuwa orodha ya waliojiandikisha zaidi ya mara
moja hupelekwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya hatua za kisheria
na kwamba Tume imefanya hivyo katika chaguzi za nyuma
ambapo katika uandikishaji uliofanyika mwaka 2015, Tume
ilibaini jumla ya wapiga kura 52,078 waliojiandikisha zaidi ya
mara moja ambapo orodha yao ilikabidhiwa kwa Jeshi la
Polisi tarehe 27 Agosti, 2015 kwa ajili ya hatua za kisheria.
“Katika uboreshaji wa Daftari wa mwaka 2020, Tume ilibaini
majina ya watu 42,301 ambao walijiandikisha zaidi ya mara
moja na orodha hiyo ilikabidhiwa kwa vyombo vinavyohusika
na makosa ya kijinai,” amesema Jaji Mwambegele.
Ameeleza kuwa baada ya kukamilika kwa uchakataji wa
Daftari, Tume huchapisha na kuweka wazi Daftari hilo chini
ya kifungu cha 24 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge
na Madiwani, Na. 1 ya mwaka 2024 ambapo wananchi
hulikagua.
“Baada ya kukamilika kwa uchapishaji wa mwisho wa Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura, vyama vya siasa hupewa nakala
tepe (soft copy), haijawahi kutokea jina likajitokeza zaidi ya
mara moja. Hivyo, hakuna uwezekano wa mtu kuandikishwa
zaidi ya mara moja na kuweza kutumia nafasi hiyo kuwa
kwenye vituo zaidi ya kimoja siku ya kupiga kura,” amesema
Jaji Mwambegele.
No comments:
Post a Comment