Watumishi wa Halmashauri na taasisi mbalimbali zilizopo Wilaya ya Magu wakishiriki zoezi la usafi wa mazingira katika eneo la hospitali ya Wilaya ya Magu ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya mashujaa Julai 25/2024.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Katibu Tawala wa Wilaya ya Magu Jubilate win Lawuo ametoa wito kwa wananchi wa Magu kuendelea kuwaenzi mashujaa kwa kua wazalendo na kulinda amani ya nchi kwani ndo msingi wa maendeleo ya Taifa letu.
Amesema watanzania wote wanatakiwa kuienzi misingi imara ya kizalendo amani na upendo iliyojengwa na waasisi wa Taifa letu ikiongozwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, misingi ambayo matunda yake tunayafaidi watanzania wote na tujipange kurithisha kwa vizazi vijavyo.
"Tumekuja hapa kwa ajili ya kumbukumbu ya wazalendo wetu waliojitoa kipindi hicho katika kulipigania Taifa letu na matunda yake tunayaona hadi leo na vizazi vyetu vutakuja kufaidi matunda haya" amesema DAS Lawuo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mohamed Ramadhani amesema Magu inawakumbuka mashujaa kwa kujitoa kwao na kusababisha Taifa kupata ukombozi ambao hadi leo watanzania wanaendelea kufaidi matunda yaliyotokana na kujitoa kwao. Funzo kwetu ni kuwa wazalendo kwa nchi yetu kama walivyokuwa Mashujaa wetu ambao walijitoa kwa hali na mali.
Aidha amesema kuwa mbali na kuwakumbuka Mashujaa waliopigania Uhuru pia usafi huo umekua ni sehemu ya kuwakumbusha Wananchi kutunza mazingira ya Wilaya kwa ajili ya afya ya Jamii huku akiwahimiza kufanya usafi kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku na sio kusubiri matukio maalumu.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa Dini Shekh wa Kata ya Isandula Majaliwa Rashid akimwakilisha Shekh Mkuu wa Wilaya ya Magu amesema viongozi wa dini wataendelea kuwakumbuka mashujaa kwa kuwaombea dua kwa mazuri waliyofanya na kusema kuwa wataendelea kuliombea Taifa liendelee kuwa na amani, upendo na mshikamano.
Kila ifikiapo Julai 25 ya kila Mwaka,Tanzania huadhimisha siku ya kuwakumbuka Mashujaa waliopoteza Maisha yao wakiutetea, Kuupigania na Kulinda Uhuru wa Tanzania. Kwa upande wa Wilaya ya Magu Siku hii pia imeambatana na Shughuli mbalimbali ikiwemo dua na sala maalumu za kuwaombea Mashujaa waliopoteza maisha yao na walio hai na kuiombea Amani ya Nchi yetu iendelee kudumu.
No comments:
Post a Comment