Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Bi. Beatrice Mwinuka akizungumza na Timu ya wataalamu ya Wizara ya Fedha na wataalamu kutoka Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) walipofika Ofisini kwake kabla ya kuanza kutoa elimu ya fedha.
Na Chedaiwe Msuya, WF, Mtwara
Serikali kupitia Wizara ya Fedha imehitimisha mafunzo ya elimu ya fedha Mkoani Mtwara ikiwa ni juhudi za kuimarisha uelewa wa masuala ya kifedha miongoni mwa wananchi.
Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko ya Mitaji na Dhamana, wametoa mafunzo hayo kwa wakazi wa mkoa wa Mtwara ambayo yalihusisha washiriki kutoka sekta mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, wakulima, wavuvi, makundi maalum na vijana kutoka katika Wilaya zote za Mkoa huo kuanzia tarehe 22 Julai,2024 na kuhitimishwa tarehe 30 Julai, 2024.
Katika kuhitimisha zoezi hilo, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Bi. Beatrice Mwinuka ameishukuru Wizara ya Fedha kwa kuwapa wananchi wa Mtwara uelewa na ujuzi wa kusimamia fedha zao kwa ufanisi, kujua mbinu bora za uwekezaji, na kujiepusha na madeni yasiyokuwa na ulazima yanayosababishwa na ukosefu wa elimu ya fedha miongoni mwa wananchi.
Mada zilizofundishwa zilijumuisha jinsi ya kupanga mipango na kuzingatia bajeti, kuweka akiba na uwekezaji, maandalizi kabla ya kustafu na namna ya kutumia mikopo kwa uangalifu. Pia, washiriki walijifunza kuhusu uwekezaji katika soko la hisa na fursa za kibiashara zinazopatikana kupitia miradi ya serikali na sekta binafsi.
Washiriki walipata nafasi ya kuuliza maswali na kushiriki mijadala iliyoongozwa na wataalamu. Mjadala huo uliwezesha watu waliofikiwa kuelewa changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika kusimamia fedha zao na kutoa suluhisho kwa vitendo.
Wananchi wameishukuru Wizara ya Fedha pamoja na wataalamu kwa mafunzo waliopatiwa hatua ambayo itafanya mabadiliko makubwa katika shughuli zao za Uzalishaji na hatimae kubadili hali za maisha yao ya kiuchumi hususan kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara.
Katika hitimisho, washiriki walipongezwa kwa kushiriki kikamilifu na kuahidi kutumia maarifa waliyojifunza kuboresha hali zao za kifedha na kiuchumi kwa ujumla.
Wizara ya Fedha imeahidi kuendelea kutoa mafunzo kama haya katika maeneo mengine ya nchi ili kufikia wananchi wengi zaidi.
Mafunzo haya yameonyesha mafanikio makubwa na matarajio ni kwamba yatakuwa na mchango mkubwa katika kuinua kiwango cha maisha ya wakazi wa Mtwara.
Ni matarajio ya Wizara ya Fedha kuwa mafunzo haya yatakuwa chachu ya maendeleo endelevu katika jamii na kubadilisha hali za maisha ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara ambao wamekuwa wakipata vipato vikubwa katika shughuli zao za uzalishaji lakini kiuhalisia hali za maisha yao yameonekana kutopiga hatua kutokana na kuwa na matumizi mabaya ya fedha kutokana na ukosefu wa elimu ya fedha miongoni mwao.
No comments:
Post a Comment